Dini ya Kiislam, imeruhusu wanaume kuoa mke zaidi ya mmoja kutokana na maandiko katika kitabu kitukufu cha Kurani na wengi wao wakiita ni sunna aliyoifanya Mtume Muhammad SAW ingawa ni kwa sheria kadhaa ila wanaume Waislamu wanaruhusiwa kuoa hadi wake wanne.
Kwa upande wa nchi za Kiislam ikiwa ni pamoja na nchi ambazo hazifungamani na dini yoyote, nyingi zinaruhusu ndoa za mitala hata hivyo, kuna nchi mbili za Kiislamu ambazo mbali na kuwa ni mataifa ya Kiislamu, ni marufuku kuoa mke zaidi ya mmoja.
Uturuki ni nchi ya kwanza ya Kiislamu kupiga marufuku ndoa za mitala huku Tunisia ikiwa ni nchi pekee ya Kiarabu ambako sheria hiyo inatumika tofauti na mawazo ya wengi ambapo nchi za kiarabu ndizo zingeongoza kwa kufuata ruhusa hii.
Katika taifa la Uturuki, marufuku hayo yaliwekwa mwaka wa 1926, uamuzi ambao haukuwa wa kidini bali wa mfumo wa kidunia.
Kwa upande wa Tunisia, ndoa za wake wengi ilipigwa marufuku mara ya kwanza mwaka 1956 na kufanyiwa marekebisho upya mwaka wa 1964.
Sheria hiyo ilitungwa miezi mitano tu baada ya Tunisia kupata uhuru kutoka kwa wakoloni wa Ufaransa ilitambulisha sheria kuwa talaka ni kesi ya mahakama iliyoamuliwa na majaji, ambayo ilimaanisha kwamba mume hawezi kumtaliki mke wake kwa urahisi, kwa maneno tu.
Hali katika mataifa mengine ya Kiislamu, ndoa za mitala ni halali lakini imedhibitiwa. Nchi hizi ni pamoja na Misri, Sudan, Algeria, Jordan, Syria, Morocco, Bangladesh, Iraq, Iran, Kuwait na Lebanon.
Taifa kama vile Indonesia, yenye idadi kubwa ya Waislamu duniani, japo haijapiga marufuku ndoa za mitala, baadhi ya majimbo yana sheria zao dhidi yake.
Mnamo mwaka wa 2008, maandamano yaliandaliwa nchini humo kupinga ndoa za wake wengi lakini matokeo yake hayakubadilisha sheria za nchi.