Iwapo unamiliki biashara ndogo, ni mzazi, mwanafunzi au mfanyakazi wa kawaida ni vyema kujiwekea muda wa kupumzika.

Kwenda likizo inatusaidia kujisikia vizuri pamoja na kuwa wafanyakazi bora zaidi. Ingawa imani maarufu ni kwamba ukichapa kazi zaidi utafanikiwa zaidi, ukweli ni kwamba unaweza kuchapa kazi na kupumzika, sana sana utafanikiwa zaidi kwa kufanya hivyo.

Kwa bahati nzuri, tunaishi kwenye nchi iliyojaa urembo na yenye sehemu nyingi za kwenda likizo. Pia, kama umeajiriwa, unapata siku 28 za kwenda likizo.

Zifuatazo ni sababu 5 za kwenda likizo.

  1. Kupunguza Msongo wa Mawazo

Wengi tunafikiri kwamba kuwa na msongo wa mawazo ni dalili ya kuchapa kazi. Ila, ukiwa na msongo wa mawazo uliopitiliza inachangia magonjwa sita yenye uwezo wa kuua magonjwa hayo ni, ugonjwa wa moyo, kansa, magonjwa ya mapafu, ajali, magonjwa ya ini na hata mawazo ya kujiua.

Kwa bahati mbaya, wengi wetu hatuwezi kuepukana na misongo ya mawazo maishani. Japokuwa unaweza kupunguza kwa kwenda gym na kula vizuri, kama unaishi kwenye mji kama Dar es Salaam ikiwa na foleni, gharama kubwa za maisha na vitu vingine vitakavyo kukera kila siku, lazima utazidiwa.

Kwenda likizo, likizo ya ukweli ambayo unajitoa katika maisha yako ya kila siku na kupumzisha akili yako, inaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa sana.

Kiukweli, badala ya kuchukua likizo ndefu mara moja kwa mwaka ni bora uende likizo fupi za siku 3 au 4 mara kwa mara kwa mwaka. Hii itakuwezesha kupunguza msongo wa mawazo kwa mfululizo ndani ya mwaka.

Sehemu za kwenda: Ikiwa unaishi mjini, tuseme Dar es Salaam, kuna hoteli nyingi zilizopo ufukweni unazoweza kutembelea. Ila, kama unataka kutoka nje ya nchi kabisa, nenda Zanzibar au Bagamoyo.

Kama huna pesa nyingi za kutumia, baki nyumbani alafu tembea mara kwa mara au nenda kwenye fukwe za umma kama Coco.

2.Kupanua mtazamo wako

Kwa kuwa tunaweka umakini kwenye maisha yetu ya kila siku, ni ngumu kuona matatizo ndani ya maisha haya, na ni ngumu zaidi kutafuta suluhisho.

Ukiwa likizo, hasa kama unasafiri kwenda mkoa, mji au nchi nyingine, unajitoa katika maisha yako ya kila siku na unajiingiza kwenye nafasi iliyo tofauti na unachokijua. Hii itakusaidia kutafakari vitu mbalimbali katika maisha yako ya kazini na kibinafsi na kuona nini cha kubadilisha na nini cha kubakisha.

Kama unaendesha biashara, nenda likizo ili ujue kama biashara inaweza kujiendesha yenyewe. Kama haiwezi, gazeti la Inc linasema kwamba “inabidi uongeza muda wa kuwawezesha wengine, kuweka mifumo bora zaidi na kuongeza uwajibikaji”.

Sehemu za kwenda:  Kuna wakala wa usafiri wazuri sana watakaoweza kukusaidia kutafuta sehemu nzuri za kwenda likizo, zilizo ndani ya bajeti yako.

Tunarudia tena, kama hutaki kutumia pesa nyingi, unaweza ukaenda kwenye likizo iliyo tofauti kidogo na ukajitolea. Au, tembelea mkoa ambao hujawahi kufika.

3.Kuongeza Ubunifu

Wengi wetu tumeona jinsi gani mfanyakazi mwenzetu amerudi kutoka likizo akiwa amebadilika kabisa na jinsi alivyokuwa kabla ya kwenda. Badala ya kuwa na uchovu na kutokuwa na motisha, amepata msisimko na ana mawazo mapya na mazuri ya kuboresha kampuni.

Ukweli ni kwamba, ubongo ukipumzika unapokea taarifa kwa ukamilifu zaidi na unaweka malengo na kufanya mazoezi, kupata ujuzi zaidi, pamoja na kutatua matatizo (bila wewe kujua). Matokeo yake ni kwamba unaboresha mawazo na ujuzi wako; unaishia kufanya kazi vizuri zaidi na pia, unakuwa mtu mzuri zaidi wa kuwa nae.

Sehemu za kwenda: Kuongeza ubunifu, tembelea sehemu za sanaa na utamaduni kwa muda wako.

4.Kuongeza Furaha

Wafanyakazi wenya furaha wanaongeza faida. Jua kwa nini hapa.

Sayansi inahusika hapa. Ukiwa likizo, mwili wako unatoa homoni ya furaha ya serotonin. Hii ina pumzisha viwango vya cortisol (hormone ya msongo wa wamazo). Mwisho wa siku, homoni nzuri zaidi zinazalishwa ndani ya mwili wako na hii inachangia mtazamo wako wa kuimarika.

Sehemu za kwenda: Sio lazima likizo iwe ya gharama kubwa au kwa muda mrefu ili iwe na faida. Ni bora uende kwenye likizo ya wikiendi kwenda sehemu isiyo na gharama kubwa badala ya kutokwenda kabisa. Lengo ni kujitoa kabisa na maisha yako ya kila siku.

5.Utendaji Bora

Utafiti uliofanyiwa na Florida State University ulionyesha kwamba watu wanaoenda likizo wanafanya kazi zaidi na wana nafasi kubwa zaidi ya kupandishwa cheo na kufanikiwa kuliko watu wasioenda likizo.

Hii inathibitisha kwamba ukijipatia muda wa kupumzika baada ya kuchapa kazi kwa muda, utaboresha utendaji kazi wako.

Lazima likizo zipewe kipaumbele

Kikubwa cha kujifunza hapa ni kwamba ukipumzika, utendaji kazi wako utakua bora na wa kasi zaidi.

Kujipumzisha si anasa, ni lazima. Na kwa kuwa tumekuonyesha umuhimu wa kwenda likizo na faida kwa afya yako ya kimwili na kiakili, pamoja na kwenye utendaji kazi, weka kipaumbele kwenye kuomba likizo.

 

 

Picha: Tayari DC Jokate Mwagelo aapishwa
Higuain, Caldara wamrudisha Bonucci Allianz Stadium