Maelfu ya Waislamu kote duniani, husherehekea siku kuu zao mbili tofauti zenye majina yaliyoshabihiana na watu wengi wamekuwa wakichanganya Siku kuu hizi mbili kutokana na uhalisia wa matamshi husika au kushindwa kutofautisha Eid ul-Fitr ni ipi na Eid al-Adha ipoje.
Dar24 Media imefanya mahojiano na Mwalimu wa Madrasat Najat Rudi, Ustaadh Ramadhan Shadadi, ambaye amefafanua uhalisia wa siku kuu hizi mbili ili kukufanya wewe ambaye hujafanikiwa kuuondoa mkanganyiko huu kupata uhalisia na uelewa.
- Eid ul-Fitr.
Maana yake ni “sikukuu ya kumaliza mfungo” na kutumiwa kuadhimisha mwisho wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Siku hii huwa ni siku rasmi ya mapumziko katika mataifa mengi yenye waumini wengi wa Kiislamu. Hata hivyo idadi ya siku za mapumziko huwa tofauti katika nchi mbalimbali.
Waislamu huanza sherehe hizi kwa kukusanyika kwa maombi ya kila mwaka ambayo hufanyika muda mfupi baada ya macheo.
Ni kawaida kuwaona Waislamu wakikusanyika katika misikiti na viwanja vya wazi kwa maoni ya pamoja.
Kabla ya ibada hiyo, huwa wanatoa sadaka kwa maskini (huitwa Zakat) ambayo ni moja ya nguzo kuu katika dini ya Kiislamu.
Ni kawaida kwa miji mikuu mataifa ya Kiislamu kupambwa sana na sherehe kubwa kuandaliwa, watoto kununuliwa nguo mpya na kupewa zawadi mbalimbali na siku hii huadhimishwa baada ya kuonekana kwa mwezi wa Shawwal.
Eid al-Adha.
Hii ndiyo sikukuu kuu zaidi ya kidini miongoni mwa Waislamu kote duniani na pia huwa ni siku ya mapumziko mataifa mengi yenye Waislamu.
Eid al-Adha maana yake ni sikukuu ya kuchinja na hutumiwa kukumbuka wakati nabii Ibrahimu alipotaka kumtoa kafara mwanawe Ismael alivyoamriwa na Allah, lakini akapewa kondoo na Mungu amtoe kafara badala ya mwanaye.
Sikukuu ya Eid ul-Adha huadhimishwa kuanzia siku ya 10 tangu kuonekana kwa mwezi wa Dhu al-Hijjah, ambapo ibada ya Hajj kwenda Mecca huanza siku mbili kabla ya Eid al-Adha na tarehe yake huthibitishwa baada ya kuoenakana kwa mwezi huo wa Dhu al-Hijjah.
Aidha, Eid al-Adha pia ina majina mbalimbali katika mataifa ya Kiislamu na wao huvalia mavazi yao mazuri na ya kupendeza katika siku hii na huenda msikitini kwa maombi, huku baadhi yao wakichinja ng’ombe, mbuzi au kondoo kukumbuka kitendo cha imani cha nabii Ibrahimu.
Waislam hutumia siku hii pia kuwapa jamaa, majirani na maskini nyama ya mnyama waliyemchinja kama moja ya Ibada na maelekezo ya Dini ya Kiislam na wao hutamkiana ‘Eid Mubarak’ neno ambalo kwa Kiarabu maana yake ni “sherehe au sikukuu njema au yenye Baraka”.