Kesho Tarehe 23 Oktoba 2021, Rais Samia Suluhu Hassan anakwenda kuwa mgeni rasmi katika kilele cha wiki ya UWT itakayoadhimishwa Ikwiriri wilayani Rufiji Mkoani Pwani na zinafanyika huko ili kumuenzi Muasisi wa Umoja huo wa Wanawake Tanzania Bibi Titi Mohamed.
Bibi Titi ni nani?
Bibi Titi Mohamed alikuwa ni mwanamke wa kwanza kujiunga na harakati mbalimbali za kupigania uhuru wa Tanganyika. Mwanzoni mwa harakati zake za kisiasa, alifanikiwa kulishawishi kundi kubwa la wanawake kujiunga pamoja naye. Kama kiongozi wa tawi la wanawake la chama cha TANU, alikuwa na jukumu la kuwashawishi wanawake kuunga mkono maoni na sera za TANU. Alikuwa mmoja wa wanawake wa kwanza wazalendo kushika nafasi za ubunge na uwaziri nchini Tanzania.
Bibi Titi Mohamed alizaliwa 1926 katikati mwa jiji la Dar es Salaam kwenye familia ya Kiislam. Kama wenzake wengi wa wakati huo, hakupata elimu rasmi, lakini alijifunza mengi kutoka kwa wazazi wake na familia yake kwa jumla.
Kwa lipi akawa maarufu?
Baada ya uhuru wa Tanganyika na katika miaka ya mwanzo ya kuundwa kwa Tanzania, Bibi Titi alipewa uwaziri chini ya uongozi wa Rais Julius Nyerere. Lakini ghafla alipoteza cheo hicho baada ya kutokubaliana na itikadi za ujamaa za Nyerere.
Mnamo 1969, pamoja na wenzake sita, wakiwemo maafisa wengine kadhaa wa kijeshi, Bibi Titi alikamatwa na kushtakiwa kwa madai ya kupanga njama za kuipindua serikali. Bibi Titi na wenzake hao walikuwa ni watu wa kwanza nchini Tanzania kukabiliwa na mashtaka ya uhaini. Baada ya kesi kusikilizwa kwa siku 127, Bibi Mohamed alihukumiwa kifungo cha maisha jela.
Hata hivyo, miaka kadhaa baadae aliachiliwa huru mnamo mwaka 1977 baada ya kusamehewa na Rais Nyerere. Alipotolewa gerezani Bibi Titi aliongoza maisha yake akiwa mpweke. Mume wake alimtelekeza wakati wa kesi, ushirika wake wa kisiasa ukanyang’anywa, na marafiki zake wengi wakamlaani
Bibi Titi Mohamed anakumbukwa vipi na UWT?
Bibi Titi anaenziwa na UWT kutokana kwa kuwa aliwakusanya wanawake katika kusimamia misimamo ya kisiasa ambayo inaendana na haki na kuwaweka wanawake mbele katika kila harakati alizoziongoza akiamini mwanamke ana nguzu sawa na mwanaume. Mara nyingi alikua akiwakusanya wanawake masaa ya jioni na kucheza michezo ya kuhamasishana umoja na nguvu ya mwanamke katika mapambano ya kisiasa.
Bibi Titi Mohamed alihutubia mikutano ya TANU miwili akihanikisha wananchi wajiunge na TANU kudai uhuru mwaka wa 1955 wakati huo haijui sura ya Julius Kambarage Nyerere inafananaje ikiwa aliingizwa TANU na waasisi wa Labour party ili aunde Idara ya Wanawake katika chama.
Wakati huo akitajwa Zaidi Tanganyika lakini mwanamke huyu Bibi Titi alivuka bahari na kuingia Zanzibar alikotoa msaada mkubwa kwa Afro Shirazi Party (ASP). Hakuishia visiwani, aliingia Kenya kuisaidia KANU ili Jomo Kenyatta atolewe kifungoni akihutubia mikutano iliyofurika watu Mombasa na Nairobi na aliwahamasisha wanawake wa Kenya kutoka jikoni waingie uwanjani katika mapambano ya kuipigania nchi yao.
Wakati huo Bi. Titi akifanya haya yote alikuwa msichana mdogo hajafika miaka 30.
Baada ya kutengana na Julius Nyerere, ikawa vigumu kupata taarifa zozote zinazomhusu Bibi Titi Mohamed. Kwa muda mrefu, serikali ilikaa kimya kuhusu mchango wake na mafanikio yake. Lakini mambo yalibadilika 1991. Katika chapisho la chama la kuadhimisha miaka 30 ya uhuru, Bibi Titi alitajwa kama “shujaa wa kike katika harakati za ukombozi”.
Tarehe 5 Novemba Bibi Titi alifariki kwenye hospitali ya Net Care Hospital mjini Johannesburg ambapo alikuwa akitibiwa.