Kocha mkuu wa Young Africans Zlatko Krmpotic, amesema kikosi chake kipo tayari kwenda kupambana katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar na mingine ya ugenini kwa sababu wanahitaji kupata alama tatu kwenye kila mchezo.

Young Africans watapambana dhidi ya Kagera Sugar Jumamosi Septemba 19, kwenye uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba mkoani Kagera mishale ya saa kumi jioni.

Zlatko amesema licha ya kupata ushindi katika mchezo uliopita, anayafanyia kazi mapungufu ya kikosi chake na anaimani ya kufanya vizuri katika michezo yao ijayo ikiwamo dhidi ya Kagera Sugar.

Kocha huyo kutoka nchini Serbia amesema anahitaji timu yake kucheza soka la kiwango cha juu na ili kufikia huko, kila mchezaji anatakiwa kuonyesha uwezo wake halisi baada ya kukamilisha programu maalumu za mazoezi alizotoa.

Amesema kwa muda mfupi amebaini wachezaji wake wanahitaji mazoezi ya kujijenga, ambayo yatawaimarisha na kuwasaidia kuingia kwa haraka katika mfumo wake ambao utawafanya wapate matokeo mazuri katika michezo inayofuata.

“Bado timu haijacheza vile ninavyotaka, ila wachezaji wangu wanapambana na kujitoa, nina imani kila siku zinavyozidi kwenda, kikosi kitakuwa imara, sasa akili yetu inajiandaa na mechi ijayo, tutahakikisha pia tunapata alama zote tatu muhimu katika mchezo huo,” amesema Zlatko.

Amesema tayari ameshawafahamu wapinzani wao Kagera Sugar baada ya kupata taarifa zao kutoka kwa wasaidizi wake ambao wamekuwa karibu wakisaidia kutelekeza majukumu yake vizuri.

“Nimepata taarifa zote kuhusu Kagera Sugar, kupitia taarifa hiyo, nimeshaandaa mbinu na mifumo tofauti ambayo inaweza kutumia kwenye mechi hiyo, nimewajua na tutajipanga kuwakabili,” Amesema Zlatko.

Young Africans wanakutana na Kagera Sugar ambao wametoka kulazimisha sare ya bila kufungana na Gwambina FC kwenye Uwanja wa Gwambina Complex wakati wao wanakumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City.

FC Barcelona yatupa ndoano kwa Depay, Pjanic atangulia Camp Nou
Chanzo ajali iliyoua watano Mtwara