Kuelekea mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho la Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Azam FC utakaopigwa baadae leo Jumatatu (Juni 12) kwenye Dimba la CCM Mkwakwani jijini Tanga, Kocha Mkuu wa Young Africans, Nasreddine Nabi ni kama amewaweka mtegoni Azam FC kwa kuwaaminisha kuwa huenda wachezaji wao watakuwa na uchovu kumbe imefichuka aliamuru mapumziko kabla ya safari ya kwenda jijini humo.
Young Africans juzi Jumamosi (Juni 10) walikuwa na maandamano ya kushangilia ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambayo yalianzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere mpaka makao makuu ya klabu hiyo, mitaa ya Twiga na Jangwani.
Tofauti na msimu uliopita ambapo sherehe za ubingwa wa Young Africans zilifanyika mpaka usiku, sherehe za ubingwa juzi Jumamosi zilimalizika majira ya saa 12 jioni ambapo imefichuka ni amri ya kocha mkuu Nabi kwa uongozi ili wachezaji wapate muda wa kupumzika kupunguza uchovu.
Mara baada ya maandamano hayo kikosi cha Young Africans jana Jumapili (Juni 11) kilisafiri kwa ndege mpaka Tanga kwa ajili ya mchezo huo unaotarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani mkoani humo.
Nabi amesema: “Tumekuwa na ratiba nyingi katika siku chache zilizopita ambazo kiukweli zimewafanya wachezaji wengi wawe na uchovu mkubwa hivyo tuna kazi kubwa ya kufanya kwenye program za utimamu wa mwili kuelekea mchezo dhidi ya Azam.
“Tunajua ni wapinzani wanaocheza mpira wa maarifa na nguvu nyingi hivyo utakuwa mchezo mgumu sana kwetu.”