Timu ya taifa ya Netiboli ‘Taifa Queens’, inatarajiwa kuingia kambini Oktoba 18, mwaka huu kujiandaa na michezo ya kuwania kufuzu fainali za Afrika.
Michezo ya kuwania kufuzu fainali hizo inatarajiwa kuchezwa Novemba 26 hadi Desemba 6, mwaka huu jijini Kampala, Uganda.
Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA), Dk. Devotha Marwa amesema, timu hiyo itaweka kambi jijini Dar es salaam au mkoani Pwani.
“Tunatarajia kuanza kambi yetu mnamo Oktoba 18, mwaka huu na inaweza kuwa katika Hosteli za Jeshi la Uokovu zilizoko Kurasini (Dar es salaam) au katika Hosteli za Shule ya Filbert Bayi (FBS) Kibaha, Pwani,” amesema.
Dk. Devotha amesema timu hiyo ya taifa itaundwa na nyota 25, waliopatikana baada ya kumalizika michuano ya Kombe la Klabu Bingwa Ligi Daraja la Kwanza, yaliyofanyika hivi karibuni katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.
“Tunatarajia kuunda kikosi imara na madhubuti ambacho tunaamini kitakwenda Kampala kushindana na siyo kushiriki tu,” amesema