Wanawake na Wanaume watakaovaa nguo fupi za kubana au kuweka suruali chini ya makalio watakamatwa na kulazimika kulipa faini ya mifuko mitano ya saruji kwa Serikali iliyo na lengo la kudhibiti mavazi yasiyo na staha.
Hatua hiyo inafuatia viongozi wa Kata ya Tandala iliyopo Wilayani Makete Mkoani Njombe kutunga sheria ndogo za kuwakata na kuwalipisha faini hiyo itakayosaidia kujenga miradi mbalimbali ya kimaendeleo ya eneo hilo.
Kwa mujibu wa Mtendaji wa kata ya Tandala Maximilian Msigwa amesema uamuzi huo umefikiwa katika vikao vya kamati na kwamba tayari sheria hiyo imeanza kufanya kazi kwa baadhi ya watu kukamatwa.
“Ni lazima tuwanyooshe warudi kwenye mstari mtu akikamatwa analipishwa mifuko mitano ya saruji kwasababu hapa tuna ujenzi wa shule yetu ya msingi Tandala hii itasaidia kuusogeza mbele” amebainisha Mtendaji.
Amesema sheria hiyo ilianza kutumika baada ya kutoa taarifa kwa wananchi ili wajirekebishe na kwamba wageni ambao hushindwa kulipa faini hiyo taratibu za kimawasiliano hufanyika na hurudishwa makwao.
“Kabla ya kuanza kwa zoezi hili wamiliki wa sehemu za starehe na wananchi kwa ujumla walipewa taarifa na wote wanaoshindwa kulipa gharama kumewekwa utaratibu ili kuwatambua na kuwarudisha makwao,” amefaanua Mtendaji.
Kwa upande wao baadhi ya Wananchi wa kata hiyo wamepongeza uamuzi wa Viongozi wao na kusisitiza matumizi sahihi ya sheria hiyo kufanyika kama ilivyokusudiwa kwani itasaidia kurejesha heshima.
“Vijana wengi wa sasa wanavaa hovyo kwa kusingizia utandawazi hii si sawa na haileti picha nzuri kwa jamii,” amesema mmoja wa wakazi wa Kijiji hicho Lususu Mbilinyi.
Tayari wito umetolewa kwa mafundi wa cherehani wa Kata hiyo kutokukubali kushona nguo fupi na zisizofaa kwa jamii na kusisitizwa waepuke kuwa sehemu ya mmomonyoko wa maadili.