Hali ya uchumi bado sio shwari nchini Afghanistan tangu kundi la Taliban kuchukua hatamu ya madaraka Agosti mwaka huu, ambapo matukio yasiyo ya kawaida yanaendelea kuripotiwa.

Kwa mujibu wa BBC, familia moja nchini humo imemuuza mtoto wao mchanga wa kike kwa $500 (sawa na Sh. 1,152,500 za Tanzania), kwa madai kuwa wanatafuta pesa ya kuwalisha watoto waliosalia ambao wako kwenye hatari ya kufa kwa njaa.

“Nimeamua kumuuza huyu mtoto wangu wa kike kwa sababu watoto wengine walikuwa wanakaribia kufa kwa njaa. Ninatamani nisingechukua uamuzi huu lakini hakuna namna,” baba wa mtoto anakaririwa.

Alipoulizwa maisha ya usoni ya mwanaye yatakuwaje, alisema mwanaye hafahamu nini kitamtokea maishani, lakini imembidi afanye hivyo kwa ajili ya ndugu zake.

Imeelezwa kuwa mnunuzi wa mtoto huyo alilipa zaidi ya nusu ya gharama kwa masharti kuwa atamalizia kiasi kilichobaki atakapokuwa anakabidhiwa mtoto pale atakapoanza kutembea.

Mnunuzi huyo alipoulizwa ana mpango gani na mtoto huyo, alisema anatarajia kuwa atakapokuwa mkubwa mwanaye wa kiume atamuoa.

Serikali ya Taliban inazunguka katika nchi zenye nguvu na mashirika ya kimataifa wakiomba misaada ya kibinadamu na chakula ili kulinusuru taifa hilo.

Ligi daraja la kwanza yamliza Amis Tambwe
Tanzania yaikingia kifua Zimbabwe