Mwanafamilia wa kundi kongwe la Hard Blasters Crew (HBC), Fanani amewataka wachezea santuli nchini kuachana na vitendo alivyoviita ‘kumuunga mkono shetani’.

Akifunguka kupitia Ladha 3600 ya E-FM, Fanani ameeleza kuwa baadhi ya wachezea santuli wamekuwa wakizipa nafasi zaidi nyimbo ambazo sio tu ziko kinyume na maadili ya kitanzania lakini pia zinapelekea watu kuunga mkono uovu.

“Nitakupa mfano, kuna wimbo wa Msaga Sumu unaitwa ‘Shemeji’, ule ni wimbo mzuri sana na unatoa mafunzo mazuri kwa watu kuishi vizuri na mashemeji kwenye jamii,” Fanani aliiambia Ladha 3600.

“Lakini kuna wimbo wa msanii mwingine kaimba kuhusu shemeji lakini anahamasisha vitendo viovu kuwa sisi huko tunapita tu, huo ndio unaona unapewa nafasi zaidi. Inakuwa kama Ma-DJ wanafanya kazi za kumpromoti Shetani,” alifunguka.

Mkongwe huyo ambaye aliunda HBC akiwa na Profesa Jay na Big Will amewataka wasanii wa Bongo Fleva kuacha kuimba nyimbo zenye matusi, ukakasi au kinyume na maadili bali wajikite katika kufanya nyimbo zinazojenga jamii bora zaidi.

IGP Sirro atoa wito kwa wanasiasa
Mpinzani wa Kagame afikishwa mahakamani Rwanda