Shirika la Chakula na Kilimo la Umoa wa Mataifa (FAO) kupitia mradi wake wa FISH4ACP limefanya mkutano wa pili wa Kikosi Kazi cha Taifa cha kukuza mnyororo wa thamani wa mazao ya uvuvi katika Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma.
Mkutano huo umefanyika mkoani Kigoma kwa lengo la kujadili na kupitisha mkakati wa uboreshaji wa mradi wa FISH4ACP na mpango wa utekelezaji wa mradi huo kama hatua ya kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya uvuvi kupitia mradi huo wa miaka mitano unaotekelezwa na FAO ambao umeanza mwezi Septemba 2020.
Hayo yameelezwa na Afisa Mtaalamu Mnyororo wa Thamani wa Uvivu na Ufugaji Viumbe Maji, kutoka FAO nchini Tanzania anayesimamia mikoa ya Katavi, Rukwa na Kigoma nchini Tanzania, Hashim Muumin amesema mradi huo unatekelezwa katika Nchi 12 za Afrika ikiwemo Tanzania .
“Mradi huu umekuja na mikakati minne ambayo ni kusaidia wachakataji wa mazao ya uvuvi wa Ziwa Tanganyika yakiwemo dagaa na migebuka, kupata masoko katika kanda hii na nje ya kanda na kutokana na utafiti tumebaini suala la mitaji kutoka katika taasisi za kifedha itakayowasaidia kuboresha shughuli zao na sisi tutawapatia mafunzo,” alisema Mratibu huyo.
Aidha Hashim alibainisha kuwa ujio wa mrad huo utasaidia kuimarisha na kujenga mazingira rafiki kwa wanawake ili kufanya shughuli zao katika nyanja ya uchakataji, wafanyabiashara na usafirishaji ili kuongeza kipato binafsi na pato la Taifa.
Naye Mteknolojia Mwandamizi wa samaki kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (sekta ya uvuvi) Masui Munda alieleza kwamba ujio wa mradio huo utachnagia kwa kiasi kikubwa kuinua sekta ya uvuvi kama ilivyo azima ya Serikali kwani uvuvi huchagiza ukuaji wa uchumi.
“ Kwa upande wa wizara sasa hivi dagaa ni zao la kimkakati kwahiyo inatumia fursa zilizopo kuinua mnyororo wa thamani wa mazao haya yanachakatwa kwa ufanisi, ubora na usalama kwa walaji ndani ya nchi na nje ya nchi kama tulivyo na masoko Canada, Austrelia na Marekani lakini bado tunataka uongeza wigo,” alileza Mteknolojia huyo.
Vile vile mchakati kutoka mwalo wa Kibirizi mkoani Kigoma Betina Tito na kiongozi wa vyama vya Uvuvi mkoa wa Kigoma, Francis John wameishukuru FAO na serikali kwa kuwapatia elimu ya uvuvi salama utakaosaidi kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya uvuvi.