Mlinda Lango wa Mtibwa Sugar Farouk Shikalo amekiri walifanya makosa makubwa katika mchezo wa Mzunguuko wanne wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Young Afrricans, uliopigwa jana Jumanne (Septemba 13), Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Mtibwa Sugar ilikubali kupoteza mchezo huo kwa kufungwa 3-0, huku ukiwa mchezo wao wa kwanza kupoteza msimu huu.
Shikalo ambaye aliwahi kuitumikia Young Africans, amesema hawakucheza vizuri na hali hiyo ilitoa nafasi kwa wenyeji wao kuwaadhibu, lakini anaamini makosa waliyoyafanya yatarekebishwa na mambo yatawanyookea katika michezo inayofuata.
“Kwa hakika hatukucheza vizuri, naweza kusema hili limetokana na uduni wa kiwango chetu dhidi ya wenyeji wetu Young Africans, nina uhakika Kocha ameona wapi tulipokosea na atakwenda kurekebisha ili tusirudie tena katika michezo inayofuata.”
“Mashabiki wanapaswa kutusamehe kwa makosa haya, tunakubali tumewaangusha sana kwa sababu walitarajia makubwa kabla ya kuanza kwa mchezo huu,”
“Hatuko mbali sana na anayeongoza Ligi kwa sasa, sisi Mtibwa tuna alama saba na wanaoongoza Ligi kwa sasa wana alama kumi, hivyo tutapambana na bado nina uhakika tupo katika hali salama ya kuendelea kupambana ili kufikia lengo letu.” amesema Shikalo
Mabao ya Young Africans katika mchezo huo yalipachikwa nyavuni na Beki wa kulia Djuma Shaban, Mshambuliaji Fiston Mayele pamoja na Kiungo Mshambuliaji Aziz Ki.