Mlinda Lango wa KMC FC Farouk Shikalo amesema bado anaamini Mshambuliaji wa Simba SC Meddie Kagere ni Mshambuliaji Bora kwake tofauti na Fistion Kalala Mayele wa Young Africans.
Shikalo ametoa tathmini hiyo huku wadau wengi wa soka la Bongo wakiamini Mayele kwa sasa hana mpinzani, kufuatia uwezo wake wa kupachika mabao kwenye Mshike Mshike wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.
Mlinda Lango huyo kutoka nchini Kenya amesema huenda wadau wengi wa soka wakashindwa kumuelewa kwa kauli yake, lakini ukweli ni kwamba umahiri wa Kagere tangu akiwa nchini Kenya unaendelea kumuweka katika nafasi ya kipekee.
Akizungumza na Azam TV, Shikalo amesema: “Hapa sina maana mbaya, ninataka kueleweka kuwa, nimecheza na Kagere katika Ligi ya Kenya na hapa Tanzania, huyu ni Mshambuliaji bora kwangu, anajua anachokifanya anapokua katika eneo la hatari.”
“Haijalishi kwa sasa ana uwezo kiasi gani, lakini anajua mbinu za kushambulia na kufanya maamuzi wakati wowote na akageuza matokeo uwanjani,”
“Mayele sio Mshambuliaji mbaya, lakini msimu huu ndio wa kwanza kwake katika Ligi ya Tanzania Bara, sijawahi kucheza naye kama ilivyo kwa Kagere na ndio maana nimesisitiza Kagere ni bora kwangu.” amesema Shikalo ambaye kabla ya kujiunga na KMC FC alikua akiitumikia Young Africans.
Kagere amewahi kuwa Mfungaji Bora katika Ligi Kuu ya Kenya kabla ya kushika nafasi hiyo katika Ligi Kuu Tanzania Bara mara mbili mfululizo msimu wa 2018/19 na 2019/20.
Msimu uliopita 2020/21 Mayele alimaliza nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji Bora Ligi ya DR Congo, akitumikia klabu ya AS Vita Club ya mjini Kinshasa.