Wakili Fatma Karume ameeleza kuwa amepokea maelekezo ya ‘mteja wake’ na anaendelea na mchakato wa kufungua kesi dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kuhusu uteuzi wa Mwanasheria Mkuu na kwamba ataisimamia kesi hiyo.
Katika malalamiko hayo, mteja wake ambaye ni Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu anapinga uteuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Adelardus Kilangi akidai kuwa umekiuka Katiba.
Shaibu anadai kuwa uteuzi huo imeenda kinyume na Ibara ya 59 ya Katiba ambayo inamtaka mteule wa nafasi hiyo kuwa wakili na mtumishi wa umma kwa kipindi kisichopungua miaka 15, na kwamba Dkt. Kilangi hana sifa hizo.
Fatma ambaye ni Rais wa Chama Cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), ameeleza kuwa wamemhusisha Rais katika kesi hiyo kwa kuwa ndiye aliyefanya uteuzi huo na kwamba wanasubiri maelekezo ya Mahakama.
“Ni kweli nimepokea maelekezo, Msajili hayupo, kwahiyo tunasubiri akirudi aisajili kesi ianze kusikilizwa,” Mwananchi wanamkariri Fatma.
Serikali kupitia kwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Amon Mpanju ameeleza kuwa bado hawajapata malalamiko hayo na hivyo hawajajua ni sheria ipi inayolalamikiwa kuwa imevunjwa.