Rais wa Chama Cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), Fatuma Karume amesema kuwa kutokana na kuwepo kwa idadi ndogo ya mawakili nchini, kwa wastani wakili mmoja hivi sasa anapaswa kuhudumia zaidi ya watu 25,000.
Akizungumza mapema leo kupitia East Africa Radio, Fatuma amesema kuwa takwimu sahihi alizonazo ofisini kwake zinaonesha kuwa mawakili wanaoendelea na kazi ya uwakili kwa mwaka huu ni takribani 2,200 pekee, tofauti na ilivyokuwa ikielezwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa ni 6,000.
Amesema kuwa hii inatokana na utaratibu wa mawakili kuwasilisha maombi ya usajili kila mwaka ili kufanya kazi za uwakili, lakini kwa mwaka jana pekee mawakili zaidi ya 600 walikataa kuendelea na usajili.
Rais huyo wa TLS amesema kuwa uamuzi wa mawakili hao kutojisajili upya, pamoja na mambo mengine ni kunatokana na changamoto walizokutana nazo kama kukamatwa walipoenda katika vituo vya polisi kuwafuatilia wateja wao na kutoridhishwa na baadhi ya mambo katika tasnia hiyo.
Wakili huyo amefafanua kuwa wingi wa wanasheria hauna maana ya idadi ya mawakili, kwani wengine kujishughulisha na kazi za kisheria na kuachana na sifa ya uwakili wa Mahakama Kuu.
Kutokana na hali hiyo, Fatuma alisema kuwa changamoto ya kuwahudumia wananchi katika kada ya sheria imeongezeka, hivyo kuwataka mawakili kuendelea kufanya kazi zao vizuri na kujituma kuwahudumia watu wengi zaidi kupata haki zao.
Imeelezwa kuwa idadi ya wananchi wanaohitaji msaada wa kisheria mahakamani ni kubwa na inazidi kuongezeka, huku wengi wakikosa fedha ya kulipia huduma za kuwa na wakili katika kesi zao.