Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) limefungua mashtaka rasmi dhidi ya raia wa Nigeria, Ramon Olorunwa Abbas maarufu kwenye mitandao ya kijamii kama ‘Hushpuppi’, kwa tuhuma za kufanya wizi wa mitandaoni na utakatishaji fedha.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, afisa wa FBI aliyefungua malalamiko hayo baada ya kukamilisha uchunguzi wa kina na kubaini mtandao wote wa Hushpuppi, wamebainika pia alifanya jaribio la kuiba fedha kwenye akaunti za benki ya timu ya Ligi Kuu ya Uingereza.
Mtuhumiwa huyo ambaye amekuwa akionesha maisha ya kifahari na anasa kwenye mtandao wa Instagram akijisifu kuwa ni mfanyabiashara mkubwa, alikamatwa Dubai akiwa na wenzake 12 na kusafirishwa hadi nchini Marekani, ambapo jana alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Chicago. Alikamatwa na polisi wa Dubai kupitia Oparesheni iliyoitwa ‘Fox Hunt 2’.
Kwa mujibu wa mashtaka yaliyofunguliwa nchini Marekani ambapo kuna wahanga wengi walioibiwa mabilioni ya shilingi na Hushpuppi na wenzake, walishuhudia kwanza maisha ya kifahari ikiwa ni pamoja na kuwa na magari ya kifahari, mavazi, ndege na majumba aliyoyaonesha mara kadhaa kwenye mtandao wa kijamii.
“Uchunguzi wa FBI umebaini kuwa Abbas alishirikiana na wenzake kutakasa mamia ya mamilioni ya dola za Kimarekani kwa kutumia mifumo ya kompyuta, ikiwa ni pamoja na mpango mmoja wa kuiba £ 100 milioni (sawa na $124 milioni) kutoka kwenye akaunti ya benki ya klabu moja ya soka la Ligi Kuu ya Uingereza,” Afisa wa FBI ameeleza.
“Pia, tumebaini kuwa Abbas na wenzake walifanya wizi uiowaathiri Wamarekani wa thamani ya fedha takribani $922,857.76, ikiwa ni pamoja na $396,050 walizoiba wakati mmoja kati yao alikuwa jijini Los Angeles, California,” aliongeza.
Wameeleza pia kuwa Februari 2019, Abbas na wenzake walifanya njama ya kuiba kiasi cha jumla ya $14.7 milioni kutoka kwenye mashirika mbalimbali ya kifedha duniani.
Wameeleza matukio mengine mengi yaliyofanywa na Hushpuppi na wenzake ambayo yaliwawezesha kuiba mamilioni ya dola za kimarekani.
Akaunti ya Instagram ya Hushpuppi yenye wafuasi zaidi ya milioni 2.3 na post zaidi ya 500 pia ilitajwa kwenye hati ya mashtaka kama sehemu ya ushahidi, ambapo imeelezwa kuwa inaonesha maisha ya anasa.
“Mamia ya taswira na picha zinazoonekana kwenye ukurasa huu zinamuonesha Hushpuppi akiwa amevalia mavazi ya gharama, akiwa kwenye magari ya kifahari, akiwa na saa za kifahari na anasa pamoja na mali nyingine ambazo zinaonesha maisha ya anasa,” imeeleza.
Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Nick Hanna ameeleza kupitia akaunti yake ya Twitter kuwa ofisi yake itahakikisha inamshughulikia Hushpuppi na watu wengine wenye mienendo kama hiyo popote walipo duniani.
Kwa mujibu wa sheria za Marekani, endapo atakutwa na hatia, Hushpuppi atakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 20 jela. Baada ya kupandishwa kizimbani Chicago, Hushipuppi atapandishwa tena kizimbani Los Angeles ambako anakabiliwa na mashtaka kama hayo.