Ukisikia mpira wa wanaume ndio umepigwa usiku huu kati ya Mabingwa wa Ulaya, FC Barcelona na mabingwa wa Europa Ligi, Sevilla.

Timu hizo zimecheza fainali ya Uefa super Cup inayoashiria kufunguliwa rasmi kwa msimu mpya wa Ulaya.

Barcelona chini ya kocha Luis Enrique wameshinda 5-4 katika mchezo uliopigwa kwa dakika 120.

Dakika 90 zilimalizika kwa sare ya 4-4 ambapo magoli ya Barca yalifungwa na Lionel Messi (6, 16), Rafinha (42), Luis Suarez (54), huku ya Sevilla yakitiwa kambani na Ever Banega (3), Jose Antonio Reyes (57), Kevin Gameiro (72 penalti) na Yevheniy Konoplyanka (81).

Dakika 30 za nyongeza wazee hao wa kazi waliendelea kutunishiana msuli, lakini Pedro Rodriguez alimaliza kazi dakika ya 115 baada ya kuandika goli la tano na la ushindi.

Barcelona wameanza msimu vizuri kwa kutwaa kombe lao la kwanza.

Pedro amefunga goli hilo muhimu wakati huu akiwa katika rada za Manchester United na baada ya mechi hii aliripotiwa kutimkia Old Trafford.

Msimu uliopita walitwaa makombe matatu (Treble) kwa maana ya La Liga, kombe la Mfalme na Uefa Champions Leagu.

Je, msimu huu watarudi rekodi hiyo?

Ndoa Mpya Ya TFF Na Vodacom Kufungwa Leo
FC Barcelona Kuwatosa Man Utd?