Majogoo wa jiji Liverpool wameripotiwa kukubali ofa ya FC Barcelona iliyomlenga kiungo mshambuliaji kutoka nchini Brazil Philippe Coutinho Correia.
Tovuti ya ESPN Brasil imeripoti kuwa, The Reds amekubali ofa ya pauni milioni 90 ambayo wanaamini inathamani ya mchezaji huyo, waliemsajili kutoka Inter Milan mwaka 2013.
Tovuti hiyo imeeleza kuwa, tayari viongozi wa pande hizo mbili wameshakutana zaidi ya mara mbili, na FC Barcelona wameafiki kulipa pesa hiyo kama ada ya uhamisho wa Coutinho.
Endapo dili la Coutinho litakamilishwa kama inavyotarajiwa, FC Barcelona watakua wameweka rekodi ya kutumia pesa nyingi katika usajili katika historia yao.
Katika hatua nyingine taarifa ambazo bado hazijathibitishwa rasmi na klabu hizo mbili imeeleza kuwa, huenda biashara ya kuuzwa kwa Coutinho ikakamilishwa siku ya jumatano na akapata nafasi ya kucheza dhidi ya Real Madrid mwishoni mwa juma hili.
Meneja wa Barca Ernesto Valverde, amepania kuwa na kikosi imara katika mchezo huo, na kama atafanikiwa kumpata Coutinho atakua amefanikisha mpango wa kuziba pengo lililoachwa wazi na Neymar aliyetimkia PSG juma lililopita.