Vinara wa Msimamo wa Ligi Kuu ya Hispania ‘La Liga’ FC Barcelona, imeachana na mpango wa kumsajili Bernardo Silva badala yake imemtolea macho Ilkay Gundogun baada ya kushindwa kumnasa Mreno huyo, wote wakikipiga Man City.
FC Barcelona ilivutiwa na Mreno huyo kwa muda mrefu lakini uhamisho wake ukagonga mwamba baada kushindwa kutoa kitita cha Pauni 60 milioni am- bayo Man City walitaka.
Sasa FC Barcelona imemuhamishia nguvu Gundogun ambaye huenda msimu huu ukawa wa mwisho kwake kukipiga Etihad, kwa mujibu wa ripoti.
Mkataba wa kiungo huyo wa kimataifa wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 32, utamalizika mwishoni mwa msimu huu na taarifa zimeripoti huenda asiongeze mkataba.
Kwa upande wa Man City ipo tayari kumwongeza mkataba wa mwaka mmoja endapo atakubali kukipiga Etihad msimu ujao wa 2023/24.
Hata hivyo, FC Barcelona iliwasiliana na wawakilishi wa kiungo huyo kuhusu mipango yao kwa ajili yake na ikaelezwa miamba hiyo imepania kumsajili katika Dirisha la usajili la kiangazi.
Gundogan alifunga bao lake la tano dhidi ya Liverpool mwishoni mwa juma lililopita, akifikisha michezo 300 tangu alipojiunga na Man City akitokea Borussia Dortmund mwaka 2016.