Imefahamika kuwa FC Barcelona ilikataa ofa ya pauni milioni 85 kutoka Manchester United kwa ajili ya uhamisho wa Mshambuliaji kinda Ansu Fati katika dirisha la uhamisho la msimu wa majira ya joto wa 2020.
Fati alifunga mabao matano na kutoa asisti nne kwenye mechi 10 katika mashindano yote mwaka jana kabla ya kupata jeraha kubwa la goti ambalo limemweka nje ya uwanja kwa miezi 10 iliyopita.
Kiwango cha nyota huyo katika msimu wa 2019-20, kiliwavutia Man United na kuamua kutuma ofa Camp Nou.
Kwa mujibu wa AS, ‘Mashetani Wekundu’ hao waliwasilisha ofa ya pauni milioni 85 kwa ajili ya huduma ya nyota huyo, wakati huo walikuwa wakijaribu kumsajili Jadon Sancho kutoka Borussia Dortmund.
Barcelona inasemekana ilikataa moja kwa moja ofa hiyo, na kikosi cha Ole Gunnar Solskjaer badala yake kikawekeza dau la pauni milioni 73 kwa Sancho katika msimu wa majira ya joto wa 2021.
Mkataba wa Fati uliopo Barcelona unafika mwisho msimu ujao wa majira ya joto, lakini Barca wanaripotiwa kuwa na imani ya kumshawishi nyota huyo wa kimataifa wa Hispania kukubali mkataba mpya.