Klabu ya Manchester United imepata ahueni ya kumsajili Mshambuliaji Kinda kutoka Hispania Ansu Fati, kufuatia Uongozi wa FC Barcelona kuthibitisha kuwa tayari kumuachia mwishoni mwa msimu huu 2022/23.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka Hispania zinaeleza kuwa Kinda huyo anawindwa vikali na timu za Ligi Kuu England huku Man United ikitajwa kuongoza katika mbio hizo.
Inaripotiwa kwamba kutokana na ufinyu wa nafasi katika kikosi cha Xavi Hernandez huenda kinda huyo akatimka kutafuta maisha sehemu nyingine msimu utakapomalizika.
Fati amefunga mabao saba na kutengeneza asisti tatu katika mashindano yote aliyocheza msimu huu na muda mwingi anasugua benchi.
Pamoja na Fati, lakini FC Barcelona huenda ikauza baadhi ya mastaa wake ili kupata fedha kutokana na matatizo ya kiuchumi yanayoikabili kwa sasa.
Ripoti zinadai FC Barcelona ipo tayari kubaki na mastaa wa zamani wa Ligi Kuu ya England iliowawasajili akiwamo Ferran Torres na Rapinha.
Mastaa Franck Kessie na Andreas Christensen huenda wakauzwa kwa sababu walijiunga na FC Barcelona bure msimu uliopita.
Kutokana na hilo Man United huenda ikaongeza nguvu zaidi kwa ajili ya Fati mwenye umri wa miaka 20, huku ikiripotiwa kwamba timu kadhaa zimepewa ofa na wakala wake Jorge Mendes.
Hivi karibuni baba mzazi wa Fati aliweka wazi kuwa mtoto wake hana furaha FC Barcelona kwa sababu hapati muda mwingi wa kucheza chini ya Xavi.
Inaaminika Fati anavutiwa na timu za Ligi Kuu England kama Arsenal na Liverpool na Man United.