Taarifa rasmi kutoka FC Barcelona imeeleza kuwa, Klabu hiyo ya mjini Barcelona imepata dili la Euro bilioni 1.5 ambalo litaiwezesha klabu hiyo kuukarabati wa Uwanja wa Camp Nou.
Barca ilikuwa imeweka tarehe ya mwisho ya mpaka Machi 31 kukamilisha mchakato wa kupata fedha kwa ajili ya mradi huo, lakini kukua kwa viwango vya riba vya dunia kulisababisha kuchelewa kwa hatua za mwisho za majadiliano hayo.
Mwishoni, wawekezaji 20 walihusika kufikia kiwango kilichohitajika ambacho kitashuhudia kukarabatiwa kwa uwanja huo na kuchukua idadi ya mashabiki 99,000 na maeneo yanayozunguka uwanja huo yakiongezwa.
Vinara hao wa Ligi Kuu ya Hispania walisisitiza kwamba katika mpango huo wa kupata fedha za kukarabati uwanja wao mali za klabu hazikuhusishwa kama dhamana na hii ni kufuatia taarifa kuwa lazima mali za klabu zihusishwe kupata fedha hizo.
“Fedha zitalipwa kwa mafungu tofauti ambapo zitalipwa kwa kipindi cha miaka mitano, saba, tisa, 20 na 24 kwa muundo unaobadilika badilika, ikiwemo muda wa kujiandaa,” ilisema taarifa ya klabu hiyo Jumatatu.
“Klabu itaanza kulipa kazi itakapokamilika, ikitumia fedha zinazopatikana katika Uwanja wa Camp Nou.”
Barcelona pia imethibitisha kuwa kampuni za Goldman Sachs, JP Morgan, JLL, Perez-Llorca, DLA Piper, Key Capital Partners, Legends na IPG 360 kuwa ni kati ya kampuni zitakazohusika kwenye uwekezaji huo mkubwa.