Nahodha na Kiungo wa FC Barcelona Sergio Busquets ataondoka klabuni hapo wakati mkataba wake na klabu hiyo utakapofikia kikomo mwishoni mwa msimu huu, imeeleza taarifa ya klabu hiyo na kuhitimisha maisha yake ndani ya miamba hiyo ya soka ya Katalunya, ambapo ameshinda mataji manane ya La Liga na matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Busquets, mwenye umri wa miaka 34, alikuwa na ofa ya kuongeza mkataba na klabu hiyo huku kocha wa Barcelona, Xavi Hernandez akieleza shauku yake ya kutaka kumbakisha kiungo huyo wa ulinzi.
Hata hivyo, baada ya miaka 18 ya kuitumikia klabu hiyo na miaka 15 akiwa kwenye kikosi cha kwanza, Busquets ameamua kuondoka na kutumia muda uliobakia wa maisha yake katika soka sehemu nyingine.
Busquets bado hajathibitisha wapi ataelekea lakini ESPN ilifichua Januari kuwa kiungo huyo amepata ofa nono kujiunga na moja ya klabu nchini Saudi Arabia.
Uko nyuma amewahi kuonyesha kutamani kucheza Ligi Kuu ya Marekani huku ikitajwa klabu ya Inter Miami kumuwania.
Mchezaji mwenzake wa zamani kwenye kikosi cha FC Barcelona, Lionel Messi ambaye kwa sasa yuko Paris Saint-Germain, pia amehusishwa na kutaka kujiunga na moja ya klabu za Saudi Arabia, ingawa baba wa mshambuliaji huyo Jumanne alikanusha uvumi huo na kwamba nyota huyo atafanya uamuzi wapi ataelekea baada ya msimu kumalizika.
Messi aliyeichezea FC Barcelona mechi 778 na Xavi mechi 767, ni wachezaji wawili walioitumikia timu hiyo mechi nyingi zaidi kumzidi Busquets ambaye ataachana na klabu hiyo kama mchezaji wa tatu aliyeichezea Barcelona mechi nyingi zaidi.
Busquets ameitumikia FC Barcelona mechi 719 na kama atacheza kwenye mechi tano za ligi zilizosalia anaweza kuongeza idadi hiyo na kufikia mechi 724.
Katika kipindi chake ameshinda mataji 31 yakiwemo mataji manane ya La Liga na matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na anatarajia kuongeza taji lingine kabla ya mkataba wake na klabu hiyo haujamalizika Juni 30.
Busquets pia ameshinda Kombe la Dunia na timu ya taifa ya Hispania, Kombe la Mataifa ya Ulaya baada ya kuichezea timu yake ya taifa mechi 143, alitangaza kustaafu soka la kimataifa baada ya fainali za Kombe la Dunia za Qatar.