FC Barcelona wameripotiwa kufikia makubaliano ya kumsajili mshambuliaji kutoka nchini Uholanzi na klabu ya Olympic Lyon ya Ufaransa Memphis Depay, kwa dau la Pauni milioni 26.
Depay anapigiwa upatu wa kutua Camp Nou, kufuatia uwepo wa meneja mpya wa FC Barcelona Ronald Koeman, ambaye amewahi kufanya kazi na mshambuliaji huyo alipokua kocha wa timu ya taifa ya Uholanzi.
Koeman anatajwa kusukuma mpango wa kusajiliwa kwa Depay, ambaye alishindwa kufanya vyema alipokua na Manchester United kuanzia mwaka 2015–2017.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26, amekua na mafanikio makubwa tangu alipotua Olympic Lyon mwaka 2017, kwani hadi sasa ameshafunga mabao 57 katika michezo 139 akiwa na klabu hiyo inayoshiriki Ligi ya Ufaransa.
Wakati Depay akipigiwa upatu wa kutua Camp Nou, FC Barcelona wamekamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji kutoka Bosnia na Herzegovina Miralem Pjanic.
Pjanic amejiunga na miamba hiyo ya Ligi Kuu ya Hispania akitokea kwa mabingwa wa Italia Juventus FC, na amekabidhiwa jezi namba 8 ya Barcelona, iliyoachwa wazi na Arthur Melo na iliyokuwa ikivaliwa na Fundi Andres Iniesta hapo awali.