Klabu ya Manchester City imekubali kumuuza mshambuliaji wake kutoka nchini Ujerumani Leroy Aziz Sané kwa Mabingwa wa Bundesliga FC Bayern Munich.
Sané anaecheza nafasi ya ushambuliaji wa pembeni, atajiunga na mabingwa hao wa Ujerumani kwa ada ya Pauni Milioni 64.8, lakini FC Bayern Munich watatanguliza kiasi cha Pauni milioni 44.7 kama sehemu ya awali ya malipo.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 24, alijiunga na Manchester City akitokea Schalke 04 mwaka wa 2016 kwa ada ya Pauni Milioni 37, na anatarajiwa kuondoka Etihad Stadium akiwa ametwaa mataji mawili ya Ligi ya England (EPL). Amecheza michezo 90 na kufunga mabao 25 akiwa na miamba hiyo ya Manchester.
Alikuwa sehemu muhimu katika kikosi cha Manchester City ambacho kilishinda mataji matatu ya nyumbani msimu uliopita, lakini msimu huu amekuwa nje kwa kipindi kirefu kutokana na jeraha la goti.
Meneja wa Manchester City Pep Guardiola juma lililopita alisema kuwa, Sané ambaye mkataba wake wa sasa ulitarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu ujao, alikataa ofa ya kandarasi mpya na anataka kuondoka.
Mshambuliaji huyo ataenda Ujerumani ndani ya saa 24 zijazo ili kukamilisha uhamisho wake.