Mabingwa wa soka nchini Ujerumani, FC Bayern Munich wameripotiwa kuwa na mpango wa kumfanya mshambuliaji wa Arsenal, Alexis Sanchez kuwa mchezaji anayelipwa pesa ndefu zaidi katika historia ya ligi ya Bundesliga endapo atakubali kutua Allianz Arena.
Taarifa kutoka nchini Ujerumani zimeeleza kuwa Bayern Munich wako tayari kumpa Sanchez mwenye umri wa miaka 28, mshahara wa Pauni 350,000 kwa juma.
Kwa sasa mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi katika ligi ya Bundesliga ni mshambuliaji kutoka nchini Poland, Robert Lewandowski anayelipwa Pauni 300,000 kwa juma.
Ikiwa usajili wa Sanchez utafanikiwa, basi Lewandowski atakuwa ameondolewa kileleni mwa orodha ya wachezaji wanaolipwa mshahara mkubwa zaidi huko Ujerumani.
Sanchez ameibuka kuwa chaguo la kwanza la wachezaji wanaohitajika FC Bayern Munich, baada ya msimu huu miamba hiyo kuchemsha kwenye michuano ya klabu bingwa Ulaya.
Ikumbukwe juma lililopita wakala wa Sanchez, Fernando Felicevich alisafiri mpaka Ujerumani kwenda kufanya mazungumzo na maofisa wa juu wa FC Bayern Munich kwa ajili ya kumtafutia changamoto mpya mteja wake.