Eva Godwin – Dodoma.
Tume ya ushindani – FCC, imeidhinisha maombi 56 ya miungano ya Kampuni kutoka sekta mbalimbali kama vile kilimo, uzalishaji, madini, mawasiliano, mafuta na Gesi.
Akizungumza na Waandishi wa habari hii leo Agosti 2, 2023 Jijini Dodoma Mkurugenzi wa tume hiyo, William Erio, amesema Maombi 51 yalipitishwa bila masharti na maombi matano yalipitishwa kwa masharti.
Amesema, “na kwa mujibu wa Sheria, maombi ya miungano yanatakiwa kushughulikiwa ndani ya siku 90, lakini kwa sasa yamekuwa yakishughulikiwa kwa wastani wa siku 75.”
Hata hivyo, amesema FCC imetoa msamaha katika mkataba mmoja uliokuwa ukififisha ushindani ambao ni kati ya Precision Air Services Plc na Kenya Airways Plc, kwa lengo la kuendeleza Sekta Ndogo ya Usafiri wa Anga Nchini.
Aidha, ameongezea kuwa FCC imechunguza Mashauri nane yanayohusu uwezekano wa kuwa na matumizi mabaya ya nguvu ya soko, ambapo moja limefungwa na mengine yako katika hatua mbalimbali za kushughulikiwa.