Scolastica Msewa, Mkuranga.

Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea mapema zaidi fedha bajeti ya mwaka 2023/24 nakufanya miradi kuanza kutekelezwa mapema zaidi.

Akifunga Baraza la Madiwani la robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/24 ya kuanzia mwezi julai hadi Septemba Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mohamed Mwela amesema mwaka huu wa fedha mafungu ya fedha za Halmashauri hiyo kiasi cha zaidi ya shilingi Bilioni 2 zikiwa ni fedha za miradi ya maendeleo ndani ya Halmashauri zimeanza kuingia tofauti na ilivyokuwa katika miaka mingine ya fedha.

Amesema, kupatikana kwa fedha hizo mapema kunafanya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo Hospitali ya Wilaya pamoja na vifaa tiba vya vituo vya afya vya huko Makumbea na Mvuleni kukamilishwa kwa wakati.

“Katika miaka mingine fedha za mwaka mpya wa fedha zilikuwa zinapokelewa katika Halmashauri hiyo hata mwezi Mei katika mwaka unaofuata lakini mwaka huu ilipofika mwezi julai kabla mwaka haujageuka tayari fedha zimeingia katika Halmashauri,” alisema Mwela.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Waziri Kombo amesema kuwa wanatarajia kukusanya zaidi ya shilingi Bilioni 13, ambapo asilimia 60 ya fedha hizo wanatarajia kuzielekeza kwenye miradi ya kimaendeleo katika halmashauri hiyo ikiwemo ujenzi wa uzio wa hospitali ya wilaya hiyo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Khadija Nasri Ali amewashukuru Watendaji wa Halmashauri hiyo kwa usimamizi mzuri wa fedha za maendeleo na hatimaye kuweza kuvuka malengo ya makisio ya bajeti hiyo na kuwaomba Watumishi mbalimbali kuendelea kuchapa kazi kwa weledi.

Leseni 441 Madini mkakati zanadiwa Uingereza
Katabazi awataka Maafisa Wakaguzi kuzingatia weledi