Azam FC wamesema kuwa hawana hofu ya mchezo wa Dar es salaam watakaocheza dhidi ya Young Africans huku wakimpa jukumu zito kiungo wao mchezeshaji Feisal Salum ‘Fei Toto’ kupambana na viungo baadhi akiwemo Pacome Zouzoua.
Timu hizo zinatarajiwa kuvaana Jumatatu (Oktoba 23) kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es salaam.
Huo ni mchezo wake wa pili kiungo huyo kuucheza wa Dar es salaam tangu ajiunge na Azam FC akitokea Young Africans ambayo alikutana nayo katika Nusu Fainali ya Ngao ya Jamii iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani iliyomalizika kwa kufungwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Kennedy Musonda na Clement Mzize.
Ofisa Habari timu hiyo, Hashim Ibwe amesema kuwa mchezo uliopita wa Ngao ya Jamii walishindwa kupata ushindi kutokana na wachezaji wao kukosa muunganiko akiwemo Fei Toto.
Ibwe amesema kuwa anaamini wachezaji hao hivi sasa wamepata muunganiko kati ya waliokuwepo zamani na wapya ili kuhakikisha wanatimiza malengo ya msimu huu.
Ameongeza kuwa mchezo huo anautaka kiungo huyo, na kikubwa anataka kulipa kisasi cha kufungwa na timu yake ya zamani katika Ngao ya Jamii.
“Fei Toto anaitaka Dabi ya Dar dhidi ya Young Africans katika mchezo wa ligi na uongozi umempa jukumu zito la kuhakikisha anatimiza majukumu yake ya uwanjani.
“Tunataka kumuona Fei Toto akionyesha ukubwa na thamani yake katika soka mbele ya viungo hao wa Young Africans ambao wenyewe wanaamini ni bora zaidi yake. “Sio huyo pekee Fei Toto, wachezaji wengine wote wanaitaka mechi hii, kwa lengo la kulipa kisasi cha kufungwa katika Ngao ya Jamii,” amesema Ibwe.