Wachezaji Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Farid Mussa Malick wamewaomba Mashabiki na Wanachama wa klabu ya Young Africans kuiombea timu yao, kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Mzunguuko wa 17 dhidi ya Geita Gold.
Mpambano huo umepangwa kuchezwa Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza Jumapili (Macho 06), huku Geita Gold FC ikiwa mwenyeji kufuatia kuuhamisha mchezo huo kutoka Uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita hadi jijini humo.
Wachezaji hao wamesema wanaamini watakua katika hali ngumu ya kupambana dhidi ya Geita Gold kutokana na wapinzani wao kuwa vizuri, ila hawana budi kuomba msaada wa dua kutoka kwa Wanachama na Mashabiki ili waweze kutimiza azma ya ushindi.
Kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’, amesema hautakuwa mchezo rahisi, lakini yeye na wachezaji wenzake, wanaahidi kupambana ili kupata ushindi, huku wakitarajia dua njema kutoka kwa Mashabiki na Wanachama.
“Mchezo utakuwa mgumu, lakini sisi kama wachezaji tutapambana na kuwapa ushindi, kikubwa watuombee dua kwa Mwenyezi Mungu tu,” amesema Fei Toto.
Naye Farid Mussa Malick, ambaye hivi karibuni aliimudu vyema nafasi ya beki wa kushoto wakati kiasili ni winga wa kushoto, amesema kwa sasa makocha wao wanarekebisha mapungufu yaliyojitokeza katika mechi dhidi ya Kagera Sugar ili mchezo unaofuata wafanye vizuri zaidi.
“Tumecheza vizuri, lakini pamoja na mazuri kulikuwa na mapungufu ambayo kwa sasa yanafanyiwa kazi ili Jumapili tupate ushindi,” alisema Farid ambaye anacheza beki ili kuziba pengo la Kibwana Shomari ambaye amesafiri na timu hadi Mwanza.
Katika mchezo wa Duru la Kwanza la Ligi Kuu msimu huu uliozikutanisha timu hizo uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, Young Africans ilichomoza na ushindi wa bao 1-0, lililofungwa na Kiungo Mshambuliaji Jesus Moloko.
Young Africans inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 42, huku Geita Gold FC yenye matokeo ya mazuri kwa siku za karibuni ikiwa na alama 21 zinazoiweka katika nafasi ya 07 kwenye msimamo.