Kiungo kutoka Visiwani Zanzibar Feisal Salum ‘Fei Toto’ amewataka wadau wa Soka la Bongo kuendelea kustahaili kinachoendelea kati yake na Uongozi wa Young Africans, lakini muda utakapowadia atafunguka kila kitu.
Fei Toto ametoa kauli hiyo baada ya saa 48 kupitia, huku Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ ikitarajiwa kutoa uamuzi wake ifikapo Mei 4, mwaka huu.
Kiungo huyo aliyeikacha Young Africans tangu Desemba mwaka 2022 amesema kwa sasa anasubiri kamati imalize kikao chake na kutoa hukumu, lakini muda muafaka ukifika atazungumza mambo yote muhimu hadharani.
“Muda ukifika nitazungumza, muda sahihi ukifika nitaweka kila kitu wazi,” Fei Toto amesema
Wakati huo huo Mkurugenzi wa Sheria wa Young Africans, Simon Patrick, amesema wanamkaribisha mchezaji huyo kufanya mazungumzo na si kupitia njia nyingine tofauti.
Simon amesema Young Africans hawamng’ang’anii nyota huyo lakini wanataka utaratibu ufuatwe, wakiruhusu mchezaji kuondoka kwa njia hii hakutakuwa mpira kwa sababu kila mchezaji ataamka asubuhi na atasema hana furaha basi anaondoka.
“Huu ni uhuni, hautakiwi kuruhusiwa katika mpira wetu, ziko njia rasmi za kuvunja mkataba na zinafahamika hadi Shirikisho la Soka Ulimwenguni (FIFA), tunachotaka kanuni za mpira zisimamiwe, tusiruhusu maharamia wanaotumia fedha. Hii si kwa Yanga tu, ni klabu zote,” amesema Mwanasheria huyo
Ameongeza kuwa Young Africans wanataka kuona sheria na taratibu zinafuatwa, kamwe hawawezi kumruhusu aondoke kiholela kwa maslahi ya heshima ya klabu hiyo.
“Young Africans ilitoa taarifa kama kuna timu inamhitaji nyota huyo basi wafike katika ofisi zetu na Fei Toto mwenye aje kukaa meza moja ili kuvunja huo mkataba,” ameongeza.
Feisal Salum aliwasilisha shauri la kutaka kuvunja mkataba wake na Young Africans kwa kulipa kiasi cha Shilingi milioni 112 kama mkataba wake ulivyosema, lakini klabu hiyo ilikataa na kufungua kesi TFF.