Kiungo wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amesema yupo fiti na tayari kuipambania timu yake itakayojitupa uwanjani kesho Jumatano (Agosti 09) kupambana dhidi ya Young Africans.
Kauli hiyo ya Fei Toto ni kama salamu kwa viungo wa Young Africans wakiongozwa na Khalid Aucho, Mudathiri Yahya, Salum Aboubakari ‘Sure Boy’ na Pacome Zouzoua ambao atakutana kwenye mchezo huo wa Ngao ya Jamii utakaochezwa Uwanja wa CCM Mkwakwani, Tanga.
Kiungo huyo amejiunga na Azam FC katika usajili huu wa dirisha kubwa akitokea Young Africans.
Fei Toto amesema amejiandaa kukabiliana na viungo wa timu pinzani ili kuhakikisha wanaifunga Young Africans na kufuzu kucheza hatua ya Fainali ya Ngao ya Jamii.
Fei Toto amesema katika mchezo huo hakuna kitu kingine wanachokihitaji zaidi ya ushindi, ambao lazima waupate ili wasonge mbele na mwisho wa siku wawe mabingwa Ngao ya Jamii.
Ameongeza kuwa, anaheshimu ubora na usajili ambao Young Africans wameufanya katika kuelekea msimu ujao, lakini hiyo haimfanyi ahofie watakapokutana nao, kwa kushirikiana na wenzake anaamini watapata matokeo mazuri.
“Malengo yangu makubwa katika msimu ujao ni kuipa makombe Azam FC, kwa kuanza tutaanza na Ngao ya Jamii kwani kombe hilo litatuongezea hamasa ya hali ya kujituma tuchukue bingwa wa Ligi Kuu Bara msimu ujao.
“Binafsi nimepanga kuisaidia timu yangu ya Azam FC kwa kuipa matokeo mazuri ya ushindi katika mchezo huo ambao tunakwenda kubeba kombe hilo la kwanza msimu huu.
“Hautakuwa mchezo mwepesi kwetu pia kwao, kwani kila timu imejianda vema mazoezini, hivyo kazi kubwa itakuwepo na kwangu nipo fiti na tayari kuipambania timu yangu ya Azam,” amesema Fei Toto.