Kikosi cha Azam FC kinajifua jijini Dar es Salaam huku kikisubiri kusepa kwenda kuweka kambi Tunisia, lakini nyota mpya wa timu hiyo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ amevunja ukimya baada ya kuanza mazoezi akisema anashukuru mapokezi aliyopata.
Feisal alitua Azam FC baada ya mzozo wake na klabu ya Young Africans kabla ya Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati na kuufanya uongozi kumpiga bei Chamazi, alianza mazoezi na timu hiyo na wenzake wapya wakiwamo makocha na kufunguka amefurahia maisha ya Azam FC.
Feisal amesema: “Nashukuru Mungu kwa wachezaji wenzangu kunipokea, nimekuwa nikizungumza vizuri nao kuhakikisha tunaisaidia timu kufika sehemu ambayo inastahili kuwa.”
Kocha mpya wa timu hiyo, Yousouph Dabo alianza na nondo mbili katika awamu ya kwanza ya maandalizi ya msimu ujao kabla ya kwenda Tunisia katika sehemu ya pili ya maandalizi hayo Dabo alianza kuandaa wachezaji kurejesha utimamu wa mwili baada ya kuwa na mapumziko ya wiki chache kisha kutokuwa waoga wa kufanya makosa kwani ni sehemu ya kujifunza.
“Tumekuwa na mazoezi ya utimamu wa mwili, lakini jambo lingine tumekuwa na mazoezi kwa ajili ya kujijenga, nini ambacho nahitaji, wakati tukiwa na mpira, niliwataka kufanya makosa kwa sababu najua wanaweza kufanya makosa wakiwa uwanjani,” amesema na kuongeza;
“Kwangu sio tatizo kwao kufanya makosa kwa sababu ni lazima itokee kwenye mpira na ni sehemu ya kujifunza,” amesema Dabo kutoka Senegal anayeondoka na timu hiyo kesho kwenda Tunisia.
Azam FC ilishika nafasi ya tatu nyuma ya Young Africans na Simba SC kwenye msimu ulioisha wa Ligi Kuu Tanzania Bara.