Mabingwa wa soka barani Ulaya, Real Madrid wamefikia hatua nzuri ya mazungumzo ya usajili wa beki kutoka nchini Brazil na klabu ya FC Porto Felipe Monteiro.
Kwa mujibu wa tovuti ya Football Espana, wababe hao wa soka mjini Madrid wamedhamiria kukamilisha usajili wa beki huyo mwenye umri wa miaka 27, baada ya kuridhishwa na uwezo wake wa kukabiliana na adui.
Wasaka vipaji wa Real Madrid walikua chanzo cha mipango ya usajili wa mchezaji huyo, baada ya kumfuatilia kwa muda mrefu na kubaini huenda akawafaa kwenye harakati zao za mapambano ya nchini Hispania na barani Ulaya msimu ujao.
Monteiro alijiunga na FC Porto mwishoni mwa msimu uliopita, akitokea nchini kwao Brazil alipokua akiitumikia klabu ya Corinthians, na amekua mchezaji anaepata nafasi katika kikosi cha kwanza cha mabingwa hao wa soka nchini Ureno.
Tayari ameshacheza michezo 24 msimu huu akiwa na The Dragoes, na amekua muhimili mkubwa wa kuitetea FC Porto katika mapambano ya nchini Ureno na barani Ulaya kabla ya kutolewa na Juventus kwenye hatua ya 16 bora siku mbili zilizopita.
Monteiro anatajwa huenda akawa mrithi wa beki wa sasa wa Real Madrid Képler Laveran Lima Ferreira (Pepe), ambaye huenda akaondoka klabuni hapo kufuatia umri kumtupa mkono.
Pepe ambaye alijiunga na Real Madrid mwaka 2007, kwa sasa ana umri wa miaka 34.