Mwimbaji aliyewahi kutikisa na ngoma kali ikiwa ni pamoja na ‘Starehe’, miaka zaidi ya 15 iliyopita, Ferooz amesema kuwa kuna watu wanaojaribu kuwabomoa wasanii wengine hata kwa kutumia uchawi na kwamba anaamini walijaribu kufanya hivyo kwake pia.
Amesema watu waliokuwa wanadai amepotea kutokana na kutumia madawa ya kulevya ni sehemu ya watu waliokuwa wanajaribu kumbomoa kwenye jamii ili asiweze kurejea tena kwenye kiwanda cha muziki lakini wameshindwa.
“Kwenye game kuna mambo mengi sana, kuna propaganda… Game sasa hivi limebadilika, muziki ambao tulikuwa tunafanya sisi zamani ni tofauti na muziki wa sasa hivi. Sasa hivi kuna vitu vingi, watu wanatumia njia nyingi mpaka uchawi, mambo mengi yanatumika kumbomoa msanii ili kumtengeneza mtu mwingine anayetengeneza brand yake,” Ferooz ameiambia Dozen Select.
“Ni haters naweza kusema walikuwa wanatumia njia hiyo kutaka kunibomoa, nionekane mimi sio na sitaweza tena kufanya muziki. Lakini wanaotumia madawa ya kulevya wasanii wenyewe wanajulikana na wameshajieleza wenyewe hadi wanaonekana wanaenda soba (sober house). Kwangu walikuwa kama wanalazimisha nikubali wakati hakuna kitu kama hicho,” ameongeza.
Katika hatua nyingine, msanii huyo amekiri kuwa walitengeneza pesa nyingi wakati wanafanya muziki na kundi la Daz Nundaz lakini mgao wa pesa hizo ulikuwa changamoto iliyobadili mambo.
Amesema kuwa wakati wanagawana sawa, baadhi ya wasanii wa kundi hilo walikuwa hawafanyi kazi kwa bidii wakiamini mgao wao upo tu, lakini walipoanzisha utaratibu wa kugawana kwa asilimia kutokana na kazi aliyofanya kila mmoja ndipo ulipozuka mzozo na lawama.
Kundi la Daz Nundaz lililokuwa linaundwa na Ferooz, Daz Baba, Sajo, Kritiki na Rarumba, lilivunjika baada ya kuachia albam zilizofanya vizuri mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Ferooz amerejea kwenye muziki baada ya kimya cha muda mrefu akiachia wimbo wa ‘Nakaza’, ambao ameeleza kuhusu tabia za binadamu alizokutana nazo alipokuwa kimya.