Mwenyekiti wa kamati ya Fiesta, Sebastian Maganga amesema tamasha hilo halitafanyika leo Jumamosi Novemba 24, 2018 kama ilivyopangwa, kwamba wananchi waliolipa viingilio watarejeshewa fedha zao.
“Tunatangaza kwa masikitiko makubwa kusitisha kilele cha msimu wa Tigo Fiesta 2018 lililopaswa kufanyika leo Novemba 24, 2018 katika viwanja vya Leaders Kinondoni Dar es Salaam, na sababu za kusitishwa kwa tamasha hili zipo nje ya uwezo wetu,” anaeleza Maganga.
Maganga ameeleza hayo leo Novemba 24, 2018 ikiwa ni saa chache baada ya manispaa ya Kinondoni kuzuia tamasha hilo kufanyika katika viwanja vya Leaders Club.
Kupitia barua inayosambaa katika mitandao ya kijamii manispaa hiyo imesema kuwa tamasha hilo limehamishiwa katika viwanja vya Tanganyika Peakers, badala ya Leaders Club.
“Tunaomba radhi kwa madhara yoyote yatakayojitokeza. Tunatambua kwamba wapenzi wa Tigo Fiesta Dar es Salaam na nje ya Dar es Salaam walishajiandaa vyema na tukio hili na zaidi ya yote wapo ambao walishanunua tiketi.”
Barua hiyo iliyoandikwa na ofisa utamaduni Manispaa hiyo jana Ijumaa Novemba 23, 2018 kwenda kwa waandaaji wa tamasha hilo, Clouds Media Group, ina kichwa cha habari kinachosema, kusitisha kibali cha kufanya Fiesta Leaders Club.
“Ofisi imepokea malalamiko ya wananchi na wagonjwa waliolazwa hospitalini kutokana na matangazo yaliyoambatana na muziki unaopigwa kwa sauti kubwa kutoka uwanja wa Leaders Club jambo ambalo linahatarisha afya za wagonjwa wakiwemo wa moyo,” imeeleza sehemu ya barua hiyo.
“Hivyo kwa barua hii nafuta kibali kilichotolewa Novemba 22, 2018 cha kufanya Fiesta uwanja wa Leaders na kuihamishia uwanja wa Tanganyika Peakers, Kawe.”
Akifafanua zaidi Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Aron Kagulumjuli amesema, “Tumelizuia (tamasha) kufanyika hapo kwani uhai wa watu ni muhimu kuliko hicho kinachotaka kufanyika.
Kagulumjuli amesema kwa hali ilivyo sasa hawawezi kuruhusu kufanyika kwa tamasha hilo viwanja vya Leaders hadi baadaye watakapojiridhisha ni salama kwa watu wengine.
“Walipokuwa wakitangaza jana hapo Leaders maeneo ya karibu kuna hospitali na watu wawili walizimia, sasa kwa njia hiyo hatuwezi kuruhusu furaha ya watu wengi ikawa majonzi kwa wengine.”