Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’ limeliondolea adhabu Shirikisho la Soka la Zimbabwe ‘ZIFA’ na limeunda kamati ya muda kusimamia mchezo wa soka nchini humo kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Uamuzi huo wa ‘FIFA’ una maana kwamba Zimbabwe itakuwemo kwenye upangaji wa ratiba ya kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2026 kesho Alhamis (Julai 13).
“Nataka kuwahakikishia Zimbabwe mna baraka kamili kutoka FIFA na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ katika kuona mchezo wa soka unafika kwenye kiwango kinachotakiwa,” amesema Solomon Mudege, Mkuu wa Maendeleo wa FIFA upande wa Afrika, kwenye mkutano na waandishi wa habari katika Jiji la Harare.
Zimbabwe ilifungiwa na FIFA Februari mwaka 2022 baada ya serikali nchini humo kuunda tume ya kusimamia mchezo wa soka na kuiweka kando ZIFA.
FIFA inapinga serikali kuingilia masuala ya soka. Kutokana na hilo, Zimbabwe iliondolewa kwenye michuano ya kuwania kufuzu kwa fainali za mataifa ya Afrika mwaka 2023 na kwa upande wa soka la wanawake mwaka 2024 lakini pia FIFA ilisitisha misaada ya kifedha kwa ZIFA.
Sababu ya serikali ya Zimbabwe kuingilia masuala ya soka ni tuhuma za mwamuzi mwanamke kufanyiwa unyanyasaji wa kijinsia na wajumbe wa kamati ya ufundi ya Zifa lakini pia tuhuma za ubadhirifu wa fedha ndani ya shirikisho hilo la soka nchini humo.