Shirikisho la soka duniani (FIFA), limeipa nafasi Tanzania kuwapa mafunzo ya juu ya ukocha wa makipa (Advanced Goalkeeping Coach Course) ikiandika historia kuwa nchi ya pili barani Afrika kwa makocha wa nafasi hiyo baada ya Botswana.

Makocha wa makipa 25 hususani wa wa timu za taifa, timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, wanahudhuria kozi hiyo inayoongozwa na Alejandro Heredia ambaye ni Mkufunzi kutoka FIFA.
Makocha hao ni Peter Manyika (Taifa Stars ya Tanzania), Saleh Ahmed (Zanzibar Heroes); Muharami Mohammed (Timu ya Taifa ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 – Serengeti Boys); Mohammed Silima (Timu ya Taifa ya Vijana Zanzibar) na Elyutery Mhoery (Timu ya Taifa ya Wanawake – Twiga Stars) na msaidizi wake ambaye pia anachezea JKT Queens, Fatuma Omary.
Wengine ni makocha maarufu wa makipa wakiwamo Juma Pondamali (Young Africans); John Bosco (Majimaji ya Songea); Salimu Tupa (Tanga); Bakari Ali Hamadi (Wete Pemba – Zanzibar); Hafidh Muhidin Mcha (Mkoani Pemba – Zanzibar); Mussa Wanena (Kagera Sugar); Juma Bomba (African Lyon), Adam Abdallah Moshi (Simba SC), Idd Mwinchumu (Azam FC) na Hussein Tade (Seeb Club-Oman/Toto African).
Pia wamo Khalid Adams (Mwadui FC); Josia Steven (Mbeya City); Herry Boymanda (Tanzania Prisons); Emmanuel Mwansile (Polisi Morogoro); Ben Kalama (Stand United); Abdallah Said (JKT Ruvu); Patrick Mwangata (Mtibwa Sugar); Augustin Malindi (Mkoa wa Kigoma); Raphael Mpangala (Ndanda FC); Salimu Tupa (Tanga) na nAbdul Mgude (Coastal Union ya Tanga).
“Mjione kwamba mmepewa kipaumbele,” alisema Heredia akiwanoa makocha hao na kuongeza: “Kinachohitajika sasa ni juhudi tu. Kozi hii haijafanyika pengine hapa barani Afrika zaidi ya Botswana. Mjue kuwa mna bahati.”
Akitoa nasaha wakati wa ufunguzi wa kozi hiyo, Makamu Rais wa TFF, Wallace Karia aliishukuru FIFA na CAF kwa namna inavyoshirikiana na TFF katika kuwapa kozio nyingi za makocha wa timu kwa wachezaji wa mbele, makocha wa makipa na waamuzi wa madaraja tofauti.
“Hakuna kipindi TFF imepata kozi za makocha nyingi za makocha kama kipindi hiki cha uongozi wa Jamal Malinzi,” anasema Karia na kuongeza: “Tumetoka kwenye kozi ya makocha wa Daraja A sasa tuko kwenu. Lengo ni Tanzania kuwe na makipa wazuri. Ninyi mtaleta makipa wazuri. Na hii ni kwa manufaa ya sasa na baadaye kwa upende wetu, timu zetu na taifa kwa ujumla.”
Karia aliwatia hamasa makocha hao wanaoshiriki kozi hiyo kuwa, mara baada ya kozi hiyo ipo siku watakwenda kuwa wakufunzi nje ya mipaka ya nchi kadhalika makocha ambao wanaweza kupata kazi mahala popote duniani hasa ukizingatia walimu wa daraja lao wako Tanzania na Botswana tu.
Kadhalika, Makamu huyo wa Rais wa TFF alielezea kuwa mpira wa miguu una changamoto nyingi na nyingine husababishwa na watalaamu hao kubweteka kwa mafanikio. “Hili ni tatizo. Tubadilike kifikra na kivitendo. Msilaze damu, kuweni active (mahiri).”

TFF Walivalia Njuga Suala La Mikataba Ya Wachezaji
Mohamed Dewji 'MO' Akabidhi Mzigo Wa Usajili Simba SC