Mkurugenzi wa Klabu ya Paris Saint-Germain, Leonardo, amesema Real Madrid inapaswa kuadhibiwa na Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’, kufuatia kumshawishi Mshambuliaji Kylian Mbappe.
Leonardo ametoa rai hiyo kwa ‘FIFA’ baada ya Rais wa Real Madrid, Florentino Perez kubainisha mapema juma lililopita kwamba, klabu yake ina matumaini makubwa ya kumsajili Mbappe wakati wa dirisha dogo la Januari (2022), lakini baadae alikanusha kwa kusema alikaririwa vibaya na vyombo vya habari.
Mbali na Perez, Mshambuliaji wa Real Madrid Karim Benzema naye aliingiza klabu yake kwenye mtego, kufuatia kusema uhamisho wa Mbappe kutua Santiago Bernabeu “ni suala la muda tu.”
Klabu ya PSG imewahi kukataa ofa kadhaa kutoka kwa real Madrid zilizohitaji kumnunua mshambuliaji huyo kinda kutoka Ufaransa (Mbappe), katika madirisha ya uhamisho ya hivi karibuni, ingawa Leonardo bado anaamini kuwa miamba hao wa Hispania wamekuwa wakimshawishi mchezaji wao, hivyo amehimiza waadhibiwe.
“Nafikiri Real Madrid imekuwa ikifanya kazi ya kumshawishi Mbappe (kwa mkataba huru) kwa muda mrefu,” amesema Leonardo akiiliambia Jarida la France Football.
“Kwa miaka miwili wamekuwa wakizungumza hadharani kuhusu Mbappe. Na kwa hili walitakiwa kuadhibiwa.
“Kutoka Real Madrid nimeona wamekosa heshima kwa Mbappe. Yeye si mchezaji wa kawaida, yeye ni mmoja wa wachezaji bora duniani.” ameongeza Leonardo.