Uongozi wa Coastal Union umeanza mazungumzo mapya ya kumuongezea mkataba mpya kocha mkuu wa kikosi hicho, Fikiri Elias baada ya kandarasi yake ya muda mfupi aliosaini kufikia tamati.

Fikiri alijiunga na kikosi hicho Februari mwaka huu akiwa ndiye kocha mkuu kwa kushirikiana na Joseph Lazaro ambaye awali alikuwa ni msaidizi wa Juma Mgunda aliyejiunga na Simba SC mwaka jana.

Katibu mkuu wa klabu hiyo, Omary Ayoub amesema ni kweli wameanza upya mazungumzo na kocha huyo na kikao cha Juni 24 watakachokaa kitakuja na mwelekeo juu ya hilo.

“Sekretarieti itakutana kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali ya klabu ikihusiana na suala la kocha, usajili mpya na wachezaji ambao tutaachana nao kila kitu tutakiweka wazi,” amesema Ayoub.

Kwa upande wa Fikiri akizungumzia hatima yake alisema lengo kubwa ambalo alipewa na viongozi ni kuhakikisha timu hiyo inasalia Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao na hilo anashukuru amelifanikisha.

“Kuhusu suala la kubaki au kutobaki hilo litategemea na maamuzi ingawa mimi niko tayari kwa lolote,” amesema Fikiri.

Kocha Nabi atoa neno la shukurani Young Africans
Serikali yafungia Hospitali 46 kwa kutoa huduma kienyeji