Mshambuliaji Mpya wa klabu ya RS Berkane ya Morocco Fiston Abdulrazack amesema bado ana deni katika soka la Bongo, baada ya kushindwa kufikia malengo yake akiwa Young Africans msimu uliopita.
Abdulrazack alisajiliwa kwa WANANCHI kama mchezaji huru msimu uliopita lakini alishindwa kumshawishi Kocha Mkuu wa Young Africans na kujikuta akiachwa mwishoni mwa msimu wa 2020/21.
Saa chache baada ya kukamilisha usajili wake RS Berkane, Abdulrazack alisema anatamani kurudi Tanzania siku moja ya maisha yake ya kucheza soka hata bure, ili aoneshe uwezo wake dimbani.
“Natamani kurudi Tz nichezee Yanga hata bure ili nioneshe uwezo wangu kwasababu naamini sikufanya waliichokuwa wanakitarajia au nikirudi nichezee Simba SC au Azam FC alafu nikutane na Yanga niwanyooshe kweli Kweli ” amesema Mshambuliaji huyo kutoka nchini Burundi.
Ifahamike kuwa Abdulrazack huenda akarejea Tanzania akiwa na RS Berkane kwa ajili ya mchezo wa hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Simba SC.
Mchezo baina ya miamba hiyo umepangwa kuchezwa Machi 13 mwaka huu, ambapo Simba SC itakua mwenyeji Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Kabla ya mchezo huo Simba SC itacheza dhidi ya RS Berkane nchini Morocco Februari 27.