Mshambuliaji kutoka nchini Burundi na Klabu ya RS Berkane Fiston Abdulrazaq amesema wanaondoka Dar es salaam-Tanzania akifahamu timu yake imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba SC.
Mshambuliaji huyo aliyeitumikia Young Africans kwa miezi sita msimu uliopita, ametoa kauli hiyo, huku akiamini Simba SC ilibebwa na Mwamuzi kutoka DR Congo Jacques Ndala Chuma akishirikiana na wasaidizi wake.
Fiston amesema RS Berkane ilicheza kwa kiwango cha juu na imedhihirisha hilo, huku ikinyimwa mkwaju wa Penati na bao halali kukataliwa kwa kisingizio cha kuotea (Offside).
“Ninachofahamu ni kwamba tumeshinda sisi sio Simba SC, kwa sababu tumenyimwa mabao mawili, moja la Penati lingine ni lile mwamuzi alilodai ni Offside.” Amesema Fiston Abdulrazaq
Bao pekee na la ushindi katika mchezo huo ulioshuhudiwa na Mashabiki 35,0000 lilipachikwa wavuni na Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Senegal Pappe Ousman Sakho na kuifanya Simba SC kufikisha alama 07 kwenye msimamo wa kundi D.
Nafasi ya Pili kwenye msimamo wa kundi hilo inashikwa na ASEC Mimosas ya Ivory Coast yenye alama 06 baada ya kuifumua USGN mabao 2-1, sawa na RS Berkane inayoshika nafasi ya tatu, huku USGN ikishika nafasi ya 04 kwa kumiliki alama 04.
Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kundi D itaendelea tena mwishoni mwa juma hili (Machi 20), ambapo Simba SC itakua ugenini ikicheza dhidi ya ASEC Mimosas nchini benin, huku USGN ikiikaribisha RS Berkane mjini Niamey-Niger.