Mshambuliaji wa FC Pyramids kutoka Misri na timu ya Taifa ya DR Congo, Fiston Mayele amefurahishwa kupangwa katika Kundi moja na timu ya taifa ya Tanzania katika makundi ya Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ zitakazochezwa mapema mwezi Januari 2024.
Tanzania katika makundi hayo imepangwa katika Kundi F pamoja na timu za taifa za Morocco, Zambia na DR Congo jambo ambalo limefurahisha Mshambuliaji huyo wa zamani wa Young Africans.
Akizungumza baada ya makundi hayo kuanikwa hahadrani juzi Alhamis (Oktoba 12) usiku Mayele amesema kuwa: Nimefurahi kupangwa pamoja na ndugu zangu kutoka Tanzania ambapo nimeishi kwa muda mrefu na sasa ni kama nyumbani kwangu kwa pili ukitoka DR Congo.
“Nafurahi kwa kuwa nitakutana na wachezaji wengi ambao tumekuwa tunafahamiana kwa muda na tumecheza wote kwa pamoja lakini pia naamini kutakuwa na ushindani mkubwa pindi ambapo tutakutana.
“Najua kuna ile kukamiana kwa kuwa tunafahamiana namna ambavyo tunacheza kuhusuiana na kundi niseme kuwa ni kundi gumu na kila timu inaweza kusonga mbele kwa kuwa kila timu ni bora na inaweza kufika mbali.”