Baada ya juhudi za kumshawishi kuendelea kuitumikia timu yao kukwama, uongozi wa Klabu ya Young Africans, umefikia makubaliano ya pamoja kumweka sokoni Mshambuliaji wao kutoka DR Congo Fiston Mayele, imefahamika.
Mayele ambaye amebakiza mkataba wa mwaka mmoja, alikuwa kwenye mvutano na uongozi wa klabu yake kwa kufanya vikao kadhaa kabla ya juzi Jumatatu (Julai 10) kufanyika cha mwisho, lakini mshambuliaji huyo raia wa DR Congo akashilia msimamo wake wakuiomba Young Africans kumuuza kwa moja kati ya klabu zinazomhitaji huduma yake.
Ingawa uongozi wa Young Africans haukuwa tayari kuweka hilo bayana, chanzo chetu ndani ya kamati yao ya utendaji, kimeeleza kuwa wamefikia uamuzi wa kumuuza kutokana na msimamo wake.
Aidha, kimesema kwamba mbali na Klabu ya Zamalek, Pyramids (za Misri) na Esperance Sportive de Tunis kuonyesha nia ya kumsajili, pia kuna klabu moja ya Saudi Arabia ipo tayari kutoa Sh. bilioni mbili za Tanzania ili kuinasa saini ya nyota huyo aliyeongoza kwa ufungaji Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika.
“Ni kweli Mayele alikutana na viongozi juu ya mustakabali wake wa kuendelea kwa msimu ujao na makubaliano yaliyofikiwa ni nyota huyo kuuzwa,” kimeeleza chanzo hicho.
Hivi karibuni Mayele aliweka wazi kuwa atakuwa na mkutano wa mwisho na uongozi wa Young Africans na juzi Jumatatu (Julai 10), walikutana na kufikia maamuzi hayo.