Mshambuliaji tegemeo wa Young Africans kwa sasa Fiston Kalala Mayele ameweka wazi anapambana kuhakikisha anaibuka na tuzo ya ufungaji bora lakini pia akilenga kuisaidia klabu yake kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Mayele ameshafunga mabao tisa katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu Tanzania Bara, akiwa nyuma ya mshambuliaji wa Namungo FC, Reliants Lusajo ambaye ametikisa nyavu za wapinzani mara 10.
Mayele ametoa tambo hizo baada ya kuwasili Jijini Mwanza, tayari kwa mchezo wa Mzunguuko wa 17 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Geita Gold FC utakaopigwa kesho Jumapili (Machi 06), Uwanja wa CCM Kirumba.
Mshambuliaji huyo kutoka DR Congo amesema malengo yake makubwa ni kuona Young Africans inapata matokeo mazuri katika kila mchezo huku akiongeza umakini wa kutumia nafasi za kufunga mabao anazopata.
“Ligi imekuwa na ushindani mkubwa, nitapambana kutimiza malengo yangu kuhakikisha natumia vizuri nafasi tunazopata kuendelea kufunga mabao na timu yangu kufikia malengo yetu,” amesema Mayele.
Amesema wakati akihitaji kuchukua tuzo ya ufungaji bora angependa kuona wanachama na mashabiki wa timu hiyo wanaendelea kufurahi.
“Kila mchezo ni mgumu na kila timu imejipanga kutafuta matokeo mazuri hasa kipindi hiki cha mechi za duru la pili, kwetu tunahitaji kuendelea kutafuta pointi muhimu ili kufikia malengo ya kutwaa ubingwa wa ligi,” amesema Mayele.
Ameongeza hana presha na kiwango chake cha kufumania nyavu na anachongalia zaidi ni kupambana katika kila mechi ili wapate kile wanachokitarajia.