Mshambuliaji kutoka nchini Burundi na klabu ya Young Africans Fiston Abdulrazak amesema kuna haja ya kuwapa heshima wapinzani wao Simba SC, hasa katika kipindi hiki ambacho wanajiandaa kucheza dhidi yao.

Young Africans itakuwa mgeni wa Simba SC Jumamosi (Mei 08), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku ikishika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufikisha alama 57.

Fiston ambaye utakua mchezo wake wa kwanza dhidi ya Simba SC tangu aliposajiliwa klabuni hapo mwezi Januari mwaka huu, amesema: “Japokuwa itakuwa mara yangu ya kwanza, lakini naona Simba ni timu nzuri inahitaji kuheshimiwa na wao watuheshimu tupo vizuri. Hapo ndipo kila mchezaji ataonyesha ufundi, tofauti na mikoani ambako kukamiana kunakuwa kwingi.”

Amesema kwa kuwa wanakutana wote ni mabingwa watapata nafasi ya kuonyesha kandanda safi tofauti na wanapocheza mikoani ambako hushindwa kufanya hivyo na kujikuta wanabutua tu.

“Ushindani unakuwa mgumu zaidi pale tunapokwenda kucheza nje ya jiji la Dar es Salaam, kutokana na viwanja vyao, pia hizo timu ambazo zipo mkiani zinatupa changamoto za kukamia mechi,” alisema na aliongeza kuwa;

“Unapocheza na timu iliyopo chini kwenye msimamo hata ikitoka sare kwao ni ushindi na mechi zinakuwa ngumu huoni sana ufundi ukifanyika kwani mipira inakuwa inabutuliwa, tofauti ukikutana na Simba,” amesema.

Mpaka sasa Simba ndiyo vinara wa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambapo wamejikusanyia alama 61, wakifuatiwa na Young Africans wenye alama 57, licha ya kwamba wamecheza michezo miwili zaidi ya Simba.

Mumbere aipeleka Simba SC nusu fainali 'CAF'
Kenyatta atoa wiki 2 mahindi ya Tanzania kuruhusiwa kuingia Kenya