Kocha wa Mabingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika RS Berkane ya Morocco Florent Ibenge, amesema anatarajia kuona Young Africans ikifika mbali zaidi kwenye michuano ya Kimataifa msimu ujao 2022/23.
Young Africans inayoshikilia Ubingwa wa Tanzania Bara kwa sasa, itashiriki Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu ujao, ikianzia hatua ya awali itakayoanza mwezi mwezi ujao.
Ibenge amesema Klabu hiyo ya Jangwani-Dar es salaam, imefanya usajili mzuri uliosheheni wachezaji wengi wenye uzoefu, hivyo itakua na kila sababu ya kupambana na kufika mbali kwenye michuano hiyo.
Amesema asilimia kubwa ya wachezaji waliosajiliwa klabuni hapo anawafahamu na amewahi kufanya nao kazi akiwa nchini kwao DR Congo.
“Asilimia kubwa ya wachezaji wa Young Africans nawafahamu, ukianzia Fiston Mayele , Yanick Bangala, Djuma Shaban, Jesus Moloko na Joyce Lomalisa ni wachezaji wakubwa, wanaijua vyema michuano ya Kimataifa, ni wabishi mno wale vijana naiona hii klabu ikifika mbali msimu ujao,”
“Naamini haitafanya makosa kwa mara ya pili, baada ya kuishia hatua ya awali msimu uliopita, hasa baadaya kuwakosa baadhi ya wachezaji wake kwa sababu za kuchelewa kwa vibali vyao vya uhamisho wa Kimataifa ‘ITC’.” amesema Ibenge
“Binafsi sitamani kukutana na hii klabu, kwa sababu nawajua wale vijana wangu, ni watu wabaya Sana wakiamua lao, niliposikia tetesi za Mayele kugoma kurudi kujiunga na timu nilisikitika namjua vizuri huyu mchezaji, nimtu muhimu sana kuwa naye kwenye timu”
“Anguko kuu la AS Vita Club ni kusambaratika kwa nyota wake kama kina Fiston Mayele , Yanick Bangala, Djuma Shaban, Jesus Moloko na Lomalisa walipoihama klabu imekufa, nimefatilia nyota walioongezwa Young Africans nawaona wakifika mbali Kimataifa, niwapongeze viongozi wao.” amesema Ibenge