Kocha wa Mkuu wa RS Berkane, Florent ibenge amesema anaendelea kujiandaa kuelekea mchezo wa Mzunguuko wa Tatu wa ‘Kundi D’ Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC.
RS Berkane iliyopoteza mchezo wake wa Mzunguuko wa Pili wa ‘Kundi D’ dhidi ya ASEC Mimosas kwa kufungwa 3-1, itakua mwenyeji wa Simba SC siku ya Jumapili (Februari 27), mjini Casablanca-Morocco.
Kocha huyo kutoka DR Congo amesema licha ya kuwa na rekodi mbaya dhidi Simba SC, haimaanishi wanakwenda kupoteza mchezo huo, ambao utakua muhimu kwa kikosi chake.
Amesema anafahamu Simba SC ina Kikosi Bora kinachoweza kupambana wakati wote, hivyo hana budi kujiandaa kikamilifu huku akiweka lengo la kuondoa unyonge dhidi ya Wababe hao wa Tanzania Bara.
“Tunaendelea kujiandaa na mchezo wetu dhidi ya Simba SC, tunaamini mchezo utakua mgumu sana, lakini tutatumia nafasi ya kuwa nyumbani ili kufanikisha lengo la ushindi. Ninajua nao wanajiandaa na mchezo huo na watakua hapa Morocco kwa siku kadhaa.”
“Ni kweli rekodi yangu dhidi ya Simba SC sio nzuri lakini haiwezi kuwa sababu ya sisi kufeli dhidi yao. Tuna nafasi nzuri ya kupambana dhidi yao, tumetoka kupoteza katika mchezo uliopita tukiwa ugenini nchini ASEC Mimosas ya Ivory Coast hivyo tunatakiwa kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani. Kwa jinsi ilivyo ni lazima tupate matokeo nyumbani.” Amesema Ibenge
Akiwa AS Vita ya nchini kwao DR Congo Ibenge alifanikiwa kuifunga Simba SC mara moja kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu wa 2018-19, huku Simba SC ikiiadhibu klabu hiyo mara tatu chini ya Kocha huyo.
Simba ilishinda dhidi ya AS Vita ya Ibenge katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu wa 2018/19, kisha ikarudia kufanya hivyo msimu wa 2020/21 kwa kuifunga nyumbani na ugenini.
Mpaka sasa Simba SC inaongoza Msimamo wa ‘Kundi D’, ikifikisha alama 4 baada ya kuibanjua ASEC Mimosas mabao 3-1 na kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya USGN ya Niger mwishoni mwa juma lililopita.
RS Berkane inashika nafasi ya tatu kwa kuwa na alama 3, ziliziotokana na ushindi wa mabao 5-3 dhidi ya USGN, kisha ikaambulia kichapo cha 3-1 kutoka kwa ASEC Mimosas mwishoni mwa juma lililopita.