Kocha Rafa Benitez ametimuliwa kazi Real Madrid baada ya kuiongoza timu hiyo kwa miezi saba tu na sasa nafasi yake inachukuliwa na gwiji wa klabu hiyo, Zinedine Zidane.

Hatua hiyo imekuja muda mfupi tu baada ya miamba hiyo YA Hispania kuitisha kikao cha dharura kufuatia kushindwa kwao kuifunga Valencia Jumapili usiku ambapo licha ya kuongoza mara mbili lakini ikaambulia sare ya 2-2.

Rais wa klabu hiyo Florentino Perez ameamua kumtimua Benitez huku Real Madrid ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo wa La Liga nyuma ya Barcelona na Atletico Madrid.

Zinedine Zidane anapanda kutoka timu B ya Real Madrid na kuchukua majukumu ya kukinoa kikosi cha kwanza ambapo ataongoza jahazi hadi mwishoni mwa msimu.

Akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari Jumatatu jioni, Perez alisema: “Rafa Benitez ni mtaalam aliyebobea na mtu wa aina yake, lakini tumeamua kumchagua Zinedine Zidane kuwa kocha mpya wa Real Madrid.”

Akizungumza na Zidane kwenye mkutano huo, Perez akamwambia: “Hii ni klabu yako, huu ni uwanja (stadium) wako.

Na unaungwa mkono na kila mmoja, kwa sasa wewe ni kocha wa Real Madrid. Najua neno ‘haiwezekani’ kwako halina nafasi”.

Perez anaendelea kuwa shabiki mkubwa wa Jose Mourinho na sasa kocha huyo wa zamani wa Chelsea anabakia kuwa suluhisho Real Madrid mwishoni mwa msimu iwapo Zidane atashindwa kuzoa mafanikio.

Akikubali ‘msalaba’ huo wa kuikochi Madrid, Zidane ambaye alishinda La Liga na Champions League akiwa kama mchezaji wa Real Madrid, alisema:

“Hii ni klabu bora duniani yenye mashabiki wengi kila kona ya ulimwengu. Nataka kuwahakikishia kuwa hadi mwishoni mwa msimu, tutakuwa na taji mkononi.”

Marko Grujic Yu Njiani Kuelekea Anfield
Madaktari Wagundua tiba ya Ukimwi, Wagonjwa wawili wapona