Hatimaye Rais wa Klabu Bingwa Barani Ulaya Real Madrid Florentino Perez amefichua siri ya kuondoka kwa Mshambuliaji Cristiano Ronaldo kwenye klabu hiyo.
Ronaldo aliihama Real Madrid mwaka 2018 na kutimkia Juventus FC ya Italia, huku akiacha maswali mengi kwa mashabiki wa soka Duniani kote.
Parez amesema wakati Mshambuliaji huyo kutoka nchini Ureno anaondoka Klabuni hapo, watu wote walisikitishwa na maamuzi yake, kwani bado alikuwa anahitajika kwa kiasi kikubwa.
Amesema Uongozi ulijaribu kukaa naye zaidi ya mara moja ili kufahamu nini tatizo, lakini walibaini FC Barcelona ndio ilikua sababu ya kuondoka kwa Ronaldo, kwani alihitaji kulipwa Mshahara mkubwa kama aliokuwa analipwa mpinzani wake Lionela Messi.
Hata hivyo kiongozi huyo wa juu wa Real Madrid amemkaribisha Ronaldo kurudi Santiago Bernabeu, lakini akamuwekea masharti ya Mshahara, kama atakubali kujiunga nao tena kwa siku za karibuni.
“Cristiano aliondoka tulipokuwa tukimuhitaji zaidi. Barcelona ndio sababu ya yeye kuondoka kwa sababu walimfanya Messi kuwa mchezaji anayelipwa vizuri zaidi duniani.”
“Sio siri kwamba Cristiano siku zote anataka kuwa hatua mbele ya Messi katika nyanja zote, lakini Sikuwa tayari kuporomosha bajeti ya Klabu ili kumfurahisha tu, akitaka kurudi tutamkaribisha, lakini kuna vigezo na masharti, Hawezi kulipwa zaidi ya wachezaji wachanga, ni mkubwa sasa. na hivi karibuni atafikia umri wa kustaafu.”
Siku za karibuni Ronaldo aliibua Songombingo Manchester United hadi kufikia hatua ya kudhaniwa huenda hataki tena kucheza ndani ya klabu hiyo, ambayo alijiunga nayo mwanzoni mwa msimu uliopita akitokea Juventus FC.
Kwa majuma kadhaa Mshambuliaji huyo aligomea mazoezi ya kikosi cha kwanza cha Manchester United, na hakuwepo katika baadhi ya michezo ya kujipima nguvu wakati wa maandalizi ya msimu mpya 2022/23.